Uhuru amtia adabu Kiunjuri
VALENTINE OBARA Na WANDERI KAMAU
MWANDANI wa Naibu Rais William Ruto, Bw Mwangi Kiunjuri Jumanne alifutwa kazi ya Waziri wa Kilimo wakati ambao wakulima kote nchini wanakumbwa na matatizo mengi.
Baadhi ya wachanganuzi walitaja hatua hiyo ya Rais Uhuru Kenyatta kama adhabu kwa Bw Kiunjuri kwa kwenda kinyume na amri yake ya kuzima siasa za mapema huku wengine wakidokeza kuwa imetokana na utenda kazi duni.
Wadadisi hao wanasema uamuzi wa Rais kumsimamisha kazi pia ni onyo kwa maafisa wengine serikalini wasiofuata misimamo ya serikali yake.
Bw Kiunjuri, ambaye aliajiriwa katika wadhifa huo mnamo Januari 26, 2018, ameibuka kuwa mmoja wa watetezi wakuu wa Dkt Ruto katika eneo la Mlima Kenya.
“Ni wazi kuwa hatua hii haikosi siasa ndani yake. Inavyoonekana, lengo ni kutoa onyo kwa mrengo wa Ruto kuhusu wanavyopinga misimamo ya serikali kuu,” akasema mchanganuzi wa siasa, Bw Holo Oiro.
Maoni sawa na haya yalitolewa na Mbunge wa Suna Mashariki, Bw Junet Mohamed: “Wale ambao hawana maono sawa na ya Rais Uhuru kupitia kwa handisheki hawana haja ya kuendelea kuwa ndani ya serikali yake.”
Kwa upande mwingine kunao wanaoamini kuwa Rais amechukua hatua hiyo kulinda masilahi ya wakulima ambao wamekuwa wakikumbwa na changamoto chungu nzima.
Karibu kila sekta ya kilimo hasa miwa, mahindi, majani chai, kahawa na maziwa zimezorota kwa kile ambacho wadau wanasema ni utepetevu na ufisadi katika Wizara ya Kilimo.
“Wakulima ndio washindi katika mabadiliko haya ya baraza la mawaziri. Hatua ya Rais kumsimamisha kazi Kiunjuri ilisubiriwa kwa muda mrefu. Amekuwa akisimamia wizara inayotumikia masilahi ya matapeli. Naamini Munya atatimiza matarajio ya Wakenya wote,” akasema Mbunge wa Nandi Hills, Bw Alfred Keter.
Nafasi yake sasa itachukuliwa na Bw Peter Munya, ambaye hadi jana alikuwa ni Waziri wa Biashara na Vyama vya Ushirika.
Lakini katika kikao cha wanahabari baadaye, Bw Kiunjuri alisema alitarajia kufutwa wakati wowote.
Hata hivyo, alikataa kufafanua ikiwa matarajio hayo yalitokana na misimamo yake ya kisiasa ya kuunga mkono Naibu Rais.
“Nashukuru kwa vile katika hotuba yake, rais alikiri kuwa sekta ya kilimo imeimarika. Sijashangazwa na hatua ya rais,” akasema.
“Nashukuru Mungu kwani huu ni mzigo mkubwa ambao nimeondolewa. Kuanzia sasa, ninafungua ukurasa mpya katika maisha yangu kwani Mungu anapofunga mlango mmoja huwa anafungua mwingine. Nitaendelea kutumikia nchi hii katika nyadhifa zingine. Siendi popote…nitakuwa humu humu,” akasema.
Wiki iliyopita, Bw Kiunjuri alijipata lawamani alipowaambia Wakenya wapige picha za nzige waliovamia maeneo mengi ya nchi na kuzituma kupitia mitandao ya kijamii kama njia mojawapo ya Wizara ya Kilimo kukabiliana na wadudu hao waharibifu.
Tangazo hilo lilichukuliwa na wengi kuwa mfano mwingine wa jinsi ameshindwa kutatua matatizo ya wakulima.
Awali, mbunge huyo wa zamani wa Laikipia Mashariki alikuwa Waziri wa Ugatuzi na Mipango kwa miaka miwili katika serikali ya Rais Kenyatta kando na kushikilia nyadhifa nyinginezo katika serikali ya Rais Mstaafu Mwai Kibaki.
Hii ni mara ya tatu Bw Munya, ambaye alikuwa gvavana wa kwanza wa Meru kuhamishwa kwani amewahi pia kuwa Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki.
Bi Betty Chemutai Maina, ambaye alikuwa Katibu wa Wizara ya Biashara, ameteuliwa kuchukua mahali pa Bw Munya katika Wizara ya Biashara. Wizara hiyo sasa itaitwa Wizara ya Viwanda, Biashara na Ustawishaji wa Ujasiriamali.
Mwingine aliyeteuliwa kuingia katika Baraza la Mawaziri ni aliyekuwa Seneta wa Nyeri na Mbunge wa Mukurwe-ini, Bw Mutahi Kagwe ambaye akiidhinishwa na bunge atakuwa Waziri wa Afya.
Bi Sicily Kariuki aliyesimamia Wizara ya Afya amehamishwa hadi Wizara ya Maji, Usafi na Unyunyizaji kuchukua nafasi ya Simon Chelugui aliyehamishwa hadi Wizara ya Leba ambayo ilikuwa ikisimamiwa na Ukur Yatani.
Rais alimwidhinisha Bw Yatani kuwa Waziri wa Fedha, wadhifa ambao amekuwa akishikilia kama kaimu tangu aliyekuwa waziri Henry Rotich aliposhtakiwa kwa ufisadi mwaka jana.
Naye Bi Raychelle Omamo amehamishwa kutoka Wizara ya Ulinzi hadi Wizara ya Masuala ya Kigeni na kubadilishana na Monica Juma.