Uhuru amwacha Ruto katika hafla
PATRICK LANG’AT, VALENTINE OBARA Na MACHARIA MWANGI
KWA siku ya pili mfululizo Jumapili, itifaki katika hafla za kiserikali ilikosa kufuatwa wakati Rais Uhuru Kenyatta alipohutubu kabla ya naibu wake William Ruto kisha akaondoka na kumuacha ahutubie waumini katika Kanisa Katoliki la Our Lady of the Rosary lililoko Ridgeways, Kaunti ya Kiambu.
Mnamo Jumamosi, Wakenya waliulizana maswali kwenye mitandao wakati Waziri wa Ulinzi, Bi Raychelle Omamo aliposoma hotuba ya Rais Kenyatta kwenye hafla ambayo Dkt Ruto alikuwepo wakati wa kutawazwa kwa Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Kisumu ya Kanisa Katoliki, Philip Anyolo.
Kulingana na itifaki, Dkt Ruto anapokuwa kwenye hafla ndiye humwakilisha rais katika wadhifa wake kama naibu wake. Ndiposa wengi walitarajia kuwa ndiye angesoma hotuba ya rais. Lakini kilichofanyika ni Dkt Ruto kuhutubu na kumwalika Bi Omamo kusoma hotuba ya rais.
Hapo jana, Kadinali John Njue, ambaye aliongoza ibada, ndiye aliyemwalika Rais Kenyatta kuhutubu akisema kiongozi wa taifa alikuwa na haraka ya kuondoka kwenda kwa shughuli nyingine.
Kadinali Njue alimwalika rais ambapo alipokezwa zawadi ya mchongo wa Maria, mamake Yesu, kisha akahutubu. Kisha rais na viongozi wengine akiwemo Dkt Ruto walitoka nje ambapo Rais Kenyatta alifungua rasmi kanisa hilo kisha akaondoka.
Dkt Ruto na wengine baadaye walirudi kanisani ambapo alihutubia waumini.
Desturi ya itifaki ni Naibu Rais kumwalika Rais, ambaye hotuba yake ndiyo huwa kilele cha sherehe zozote zile anazohudhuria. Lakini jana ilishangaza Rais kualikwa na Kadinali Njue mbele ya Bw Ruto na pia kuhutubu kabla ya naibu wake.
Kwenye hotuba zao, viongozi hao wawili walitoa wito wa umoja na amani.
“Mahali watu wanapanda chuki, tutapanda upendo. Mahali wanapanda migawanyiko, tutapanda umoja kwani mwishowe hiyo ndiyo itatuwezesha kuendeleza mbele nchi yetu,” akasema rais.
Aliongeza: “Naomba kila mmoja wenu kujiunga nasi katika harakati hizi za kuleta amani na kujenga taifa lenye ufanisi na umoja.”
Kwenye hotuba yake, Dkt Ruto alionekana kuhimiza kutulizwa kwa joto la kisiasa lililosababishwa na mjadala kuhusu azma yake ya kumrithi Rais Kenyatta 2022.
Mjadala huo ulitokota baada ya aliyekuwa Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Jubilee aliyejiuzulu, Bw David Murathe kudai hapakuwepo maelewano yoyote kwamba jamii ya Mlima Kenya itamuunga mkono Dkt Ruto ifikapo 2022.
“Mimi kama msaidizi mkuu wa rais nilikula kiapo mbele za Mungu na mwanadamu kumsaidia bosi wangu, Rais Kenyatta kufanikiwa katika jukumu lake na nimefanya kazi hii kwa uaminifu,” akasema Dkt Ruto.
Alipuuzilia mbali madai ya baadhi ya wandani wake kutoka Mlima Kenya akiwemo Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria na mwenzake wa Bahati, Kimani Ngunjiri kwamba eneo hilo limetengwa kimaendeleo.
Baadaye Naibu Rais alielekea Naivasha, Kaunti ya Nakuru kwa ibada nyingine kanisani ambapo aliandamana na magavana wawili, seneta na wabunge zaidi ya 40 kutoka kaunti za eneo la Mlima Kenya na akawataka viongozi wamheshimu rais.
Baadhi ya viongozi walioandamana naye ni Gavana wa Kiambu, Bw Ferdinand Waititu na mwenzake wa Nakuru, Lee Kinyanjui na Seneta wa Nakuru Susan Kihika.