HabariSiasa

Uhuru apondwa Mlima Kenya

May 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

ERIC WAINAINA na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta Jumatatu alishambuliwa vikali na viongozi, wafanyabiashara, wanamuziki na wakazi wa ngome yake ya kisiasa ya Mlima Kenya, kutokana na sera ambazo wakazi wanasema zinatatiza shughuli zao za kupata pesa.

Mbunge wake Moses Kuria (Gatundu Kusini) na aliyekuwa gavana wa Kiambu, William Kabogo walimshauri kiongozi wa taifa kuchukua hatua za haraka kurekebisha hali ya nchi.

Kwenye vituo vya redio vya lugha za kiasili, mitandao ya kijamii na kwenye muziki, wakazi wamekuwa wakieleza hasira kwa kile wanasema ni hatua za serikali za kuwavuruga kiuchumi.

Mwanamuziki Ng’ang’a wa Kabari alichomoa kibao, Ni Thirikari (Ni Serikali), ambacho kinashutumu vikali serikali kwa matatizo yanayokumba nchi, pamoja na ufisadi wa kupindukia.

Hatua ambazo zimewakera wakazi ni pamoja na kuzuiliwa kwa mizigo ya wafanyibiashara wanaoagiza bidhaa kutoka ng’ambo, ambao wengi hufanya biashara maeneo ya Nyamakima na Gikomba jijini Nairobi.

Habari za kupiga marufuku uagizaji wa vipuri vilivyotumika kutoka ng’ambo hapo jana ziliongezea manung’uniko ya wakazi.

Wafugaji wa ng’ombe wa maziwa nao walikasirishwa na sheria iliyopendekezwa, lakini ikaondolewa baadaye, ya kupiga marufuku uuzaji rejareja wa maziwa. Sheria hiyo ilionekana na wengi kama mbinu ya kusaidia kampuni fulani kubwa za kupakia maziwa.

Pia sheria iliyopendekezwa ya kupiga marufuku utumizi wa mbolea ya mifugo kwenye kilimo ilizua pingamizi kali katika eneo hilo ambalo wengi wa wakazi wake ni wakulima na wafugaji.

Ubomoji wa vibanda katika miji, unyanyasaji wa wahudumu wa matatu na kukosa kufufua sekta za kahawa, viasi na majani chai pia ni mambo ambayo wakazi wamekuwa wakilalamika kwa wingi.

Hapo jana, aliyekuwa gavana wa Kiambu, William Kabogo alimkosoa Rais Kenyatta akisema sera ambazo zinachukuliwa na serikali yake zinanyanyasa wananchi wa kawaida badala ya kuwasaidia kujiinua kiuchumi.

Akihojiwa kwenye redio ya Kameme FM, Bw Kabogo alisema maafisa serikalini wanaweka sera na sheria zinazolenga kusaidia watu binafsi wala sio nchi.

Alikosoa serikali kwa kuzuiliwa bandarini kwa mizigo iliyoagizwa na wafanyibiashara wadogo wadogo akisema serikali yenyewe ndiyo ya kulaumiwa kwani ni taasisi zake ambazo zilitoa vyeti vya bidhaa hizo kuletwa nchini.

Bw Kabogo alisema sera nyingi za serikali ya Jubilee hazichangii katika kubuniwa kwa nafasi za kazi mbali zinachangia watu kufutwa kazi.

Alimwambia Rais Kenyatta kuwa ataacha sifa mbaya atakapostaafu iwapo hatachukua hatua za kurekebisha mazingira ya uchumi, kupigana na ufisadi na kuwakomboa Wakenya kutokana na umaskini.

Bw Kuria naye alisema serikali iliwadaganya wapigakura wa eneo la Mlima Kenya na akamtaka Rais Uhuru Kenyatta kuvunja baraza lake la mawaziri akisema wanampotosha.

Bw Kuria alisema mawaziri kutoka eneo hilo wamekuwa wakimdanganya Rais kwamba mambo yako sawa mashinani, ilhali watu wanateseka, hasa kwa sababu ya sera za serikali zinazofanya watu kushindwa kuendeleza biashara au kuhujumu shughuli za kiuchumi nchini.

Alimtaja Waziri wa Biashara na Viwanda Peter Munya, Sicily Kariuki (Afya), Mwangi Kiunjuri (Kilimo) na James Macharia (Uchukuzi) kama kiini cha matatizo ya wakazi wa Mlima Kenya.

Bw Kuria alisema licha ya kushikilia wizara muhimu katika serikali ambazo zinahusiana na shughuli za kiuchumi za wakazi wa eneo hilo, mawaziri hao wameshindwa kubuni sera za kuimarisha shughuli hizo na wamefanya watu wengi kuteseka.

“Katika wizara zote muhimu Rais Uhuru Kenyatta ameteua watu wetu na kwa hivyo watu wanaotutesa ni wale kutoka eneo letu na sio maeneo mengine,” Bw Kuria alisema.

Alitoa mfano wa eneo la Nyamakima jijini Nairobi ambako wafanyabiashara wadogo wadogo, wengi wao kutoka eneo la Mlima Kenya, wamefutwa kazi na wengine kufunga biashara kwa sababu hakuna bidhaa za kuuza kwa sababu ya sera za serikali.

Alisema wafanyabiashara wanafaa kuruhusiwa kuendelea kuingiza bidhaa kutoka nje bila vizingiti vingi kwa kisingizio cha kukabiliana na bidhaa ghushi.