HabariSiasa

Uhuru ataachia Wakenya deni la Sh7 trilioni akiondoka mamlakani

September 26th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

CONSTANT MUNDA na PETER MBURU

RAIS Uhuru Kenyatta atakuwa amekusanya takriban Sh2.13 trillioni za madeni kufikia wakati atakapomaliza muhula wake, Agosti 2022. Hii ni kulingana na utabiri wa Wizara ya Fedha, ambao unaashiria hatari zinazokumbana nazo pesa za mlipa ushuru.

Kulingana na utafiti wa wizara hiyo, madeni ya umma yatakuwa yamegonga karibu 7.17 trillioni hapo Juni 2022, kutoka takriban Sh5.04 trilioni kufikia Juni mwaka huu.

Ikiwa hilo litatimia, Rais Kenyatta atakuwa amekopa angalau deni la Sh5.27 trilioni ili kutekeleza manifesto zake ndani ya kipindi cha miaka 10, baada ya kuchukua hatamu za uongozi wakati deni lilikuwa Sh1.8 9trilioni kufikia Juni 2013.

Serikali ya Jubilee imezidisha matumizi tangu 2013 ili kutengeneza barabara, reli, madaraja na vituo vya umeme vya hadhi, jambo ambalo limezidisha ukopaji ili kulipia mapungufu kwenye bajeti.

Kuongezeka kwa madeni hayo kumeifanya Kenya kuanza kutumia zaidi ya nusu ya ushuru wa taifa kulipa madeni, na kuwacha pesa chache za kutumika kwa ujenzi wa barabara, nyumba za gharama ya chini na kufadhili sekta ya afya ambayo ina shida tele.

Deni la umma lilikuwa Sh5.04 hadi juni Mwaka huu, idadi ya juu kutoka Sh4.41 trilioni kufikia Juni 2017, Sh3.62 trilioni hadi Juni 2016, Sh2.83 trilioni mnamo Juni 2015, Sh2.37 trilioni Juni 2014 na Sh1.89 trilioni Juni 2013.

Wataalam wa masuala ya kiuchumi sasa wamesema kuwa sababu ya kuongezeka kwa madeni ya serikali imechangiwa na serikali kuweka bajeti kubwa na malengo yasiyowezekana, na ambayo mwishowe mengi hayatimiliki.

Bw Jibran Quereishi, mtaalamu wa kiuchumi kutoka benki ya Stanbic alisema kukopa huko kupita kiasi kumeizidishia serikali hamu ya kuwa ikikopa kila wakati, hata bila kukagua ikiwa madeni hayo yanatumika kwa njia za manufaa.

“Pale inapoweka bajeti kubwa hata kuliko mipango ya matumizi, serikali inaishi kudhani kuwa itatekeleza hata wakati hakuna pesa za kufanya hivyo,” Bw Quereishi akasema.

Waziri wa fedha Henry Rottich anapanga kutumia Sh870.5 bilioni kulipa madeni mwaka huu, kiwango cha juu kutoka Sh435.7 bilioni zilizotumika kwa shughuli hiyo mwaka wa fedha uliopita, na kutoka kwa ushuru wa Sh1.76 trilioni unaotarajiwa kukusanywa.

Kenya imezidisha fursa ya kupokea mikopo ya riba ya chini kimataifa tangu uchumi wake ulipopanda Septemba 2014, hali ambayo imelifanya taifa kukimbilia mikopo ghali na ya muda mfupi kutoka kwa mashirika ya kimataifa.

“Wasiwasi unaoibuka ni kuwa hamu ya serikali kukopa inaonekana haitaisha wakati wowote hivi karibuni, hali ambayo inaweza kulisukuma taifa kwa madeni yasiyoweza kulipika,” ofisi ya bajeti bungeni ikasema katika ripoti yake iliyotolewa mwezi uliopita.