HabariSiasa

Uhuru awaka lakini Moses Kuria akaa ngumu

January 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

VALENTINE OBARA, MOHAMED AHMED Na LUCAS BARASA

RAIS Uhuru Kenyatta Jumatatu aliwajibu kwa ukali wanasiasa kutoka ngome yake kuu ya kisiasa ya Mlima Kenya, ambao wamemkosoa kwa madai ya kupuuza eneo hilo kimaendeleo.

Akionekana mwenye ghadhabu kuu, Rais Kenyatta aliwataja wanasiasa hao kama “washenzi” na kuwaambia wenyeji wa Mlima Kenya kuwa wasitarajie awapendelee kimaendeleo kwa msingi kuwa anatoka eneo hilo.

Kulingana na Rais Kenyatta, imani kwamba eneo fulani linastahili maendeleo zaidi kwa vile ‘mwana wao’ yuko mamlakani imepitwa na wakati kwani kila pembe ya nchi ina haki sawa.

“Tunataka nchi ambayo kila mwananchi ana haki ya kupata maendeleo bila kujali mahali kiongozi anakotoka. Hiyo ndiyo siasa tunayotaka katika nchi hii. Kwa hivyo hawa ‘washenzi’ waachane na mimi. Wale ambao hawataki kujua Kenya imebadilika shauri yao, wakae kando tusonge mbele,” akasema akiwa Mombasa.

Matamshi ya Rais Kenyatta yaliwalenga viongozi kadhaa wa eneo hilo wakiongozwa na mbunge wake, Moses Kuria (Gatundu Kusini) na Kimani Ngunjiri (Bahati) ambao wamelalamika kuwa eneo hilo limebaki nyuma kimaendeleo chini ya uongozi wake.

Muda mfupi baada ya matamshi ya rais, Bw Kuria alijibu akisisitiza kwamba hatabadili msimamo wake wa kupigania maendeleo ya Mlima Kenya.

Kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook, mbunge huyo alisema: “Ninaamini Mlima Kenya pia unahitaji maendeleo sawa na eneo lingine lolote. Kwa sasa hilo halifanyiki.”

“Rais amesema ukweli kuwa kila pembe ya nchi inahitaji maendeleo. Lakini hatuna mradi wowote mkubwa eneo la Mlima Kenya huku maeneo mengine ambayo hayakumpigia kura yakiwa na miradi ya mabilioni ya pesa,” akaongeza Bw Kuria

Bw Kuria aliungwa mkono na wengi kwenye mitandao ya kijamii chini ya heshtagi #teamwashenzi, ambapo wakazi wa Mlima Kenya walieleza hasira dhidi ya Rais Kenyatta wakisema hafahamu wanavyoteseka.

Wengine waliandika: “Haha ni gute” (hapa ni kupoteza) na baadhi wakisema amehama Jubilee na kujiunga na chama cha ODM.

Kulingana na Bw Kuria na Bw Ngunjiri, umaskini miongoni mwa wakazi wa Mlima Kenya umeongezeka chini ya uongozi wa Rais Kenyatta licha ya eneo hilo kumuunga mkono kwa dhati.

“Mimi si mtu ambaye anatishika haraka hasa nikijua njia niliyotenga, na pale ambapo ninataka kuona Wakenya wamefika,” akasema.

Kwenye hotuba yake, Rais Kenyatta alitetea mwafaka wake na Bw Odinga na akakemea wale wanaoingiza siasa za urithi wa 2022 katika maelewano hayo.

Alirejelea kwamba mwafaka wao ulinuiwa kufanikisha maendeleo yatakayoboresha maisha ya wananchi katika nyanja mbalimbali ikiwemo huduma bora za afya kwa bei nafuu, usalama, usambazaji wa maji safi, uzalishaji chakula cha kutosha, ujenzi wa nyumba za bei nafuu na kudumisha amani kitaifa.

“Tamaa ya uongozi ni sawa lakini haiwezi kuzidi shida za wananchi. Hakuna nchi ambayo inaweza kuendelea ikiwa tamaa ya kiongozi ndiyo inatawala kuliko shida za mwananchi,” akasema.

Kwa upande wake, Bw Odinga alipuuzilia mbali viongozi wa Jubilee wanaodai ananuia kutumia mwafaka wake na Rais Kenyatta kuvuruga chama hicho huku akikemea kampeni za urais za mapema.

“Mambo ya 2022 yatafika. Kutakuwa na wanaume na akina mama ambao watasimama lakini sasa bado tuko 2019. Hawa jamaa tunawaambia tupatieni nafasi tuendeleze Kenya mbele kwanza,” akasema.

Wandani wa Naibu Rais William Ruto ndio wamekuwa katika mstari wa mbele kudai Bw Odinga amenuia kutumia mwafaka wake na Rais Kenyatta kumharibia Naibu Rais nafasi ya kushinda urais ifikapo 2