Uhuru awataka wabunge wa Jubilee wasiounga mkono serikali wang'atuke
Na CHARLES WASONGA
RAIS Uhuru Kenyatta amewaonya wabunge waasi wa Jubilee ambao hupinga misimamo ya chama hicho na ajenda za serikali bungeni.
Rais alisema kuwa wabunge kama hao wanafaa kujiuzulu ikiwa hawataki kuunga mkono agenda za chama hicho tawala.
Duru ziliambia Taifa Leo Dijitali kwamba kiongozi wa taifa alitoa onyo hilo Jumatano katika Ikulu ya Mombasa kwenye kikao cha kuratibu ajenda zake bungeni mwaka huu.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Naibu Rais William Ruto, maspika Justin Muturi (Bunge la Kitaifa) Ken Lusaka (Seneti) na Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju.
Wengine waliokuwepo ni uongozi wa mrengo wa serikalini bungeni; Adan Duale (Kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa), Kipchumba Murkomen (Kiongozi wa wengi katika seneti), Moses Cheboi (Naibu Spika bunge la kitaifa), Profesa Kithure Kindiki (Naibu Spika Seneti) na kiranja wengi katika seneti Irungu Kang’ata.
Rais aliukaripia uongozi wa Jubilee bungeni kwa kufeli kuwadhibiti wabunge wa chama hicho, akitoa mfamo wa kisa ambapo nusra Mswada wa Fedha uangushwe.
Hii ni baada ya baadhi ya wabunge wa Jubilee kuungana na wenzao wa upinzani kupinga kuanzisha kwa ushuru wa thamani ya ziada (VAT).
Hata hivyo, njama zao ziligonga mwamba kutokana na hila za wabunge watiifu kwa Rais Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga ambapo waliondoka nje na kupunguza idadi ya wabunge hitajika kubatilisha pendekezo la Rais kwenye mswada huo.
Baada ya wabunge wa Jubilee waliopinga mswada huo ni James Lomenen (Turkana Kusini), Catherine Waruguru (Mbunge Mwakilishi wa Laikipia), Didmus Barasa (Kimilili), Cornel Serem (Aldai), kati ya wengine.
Ilidaiwa wengi wa wabunge wa Jubilee waliopinga mswada huo ni wale wa mrengo unaounga mkono azma ya Naibu Rais William Ruto kuingia Ikulu 2022, maarufu kama wanachama wa “Team Tangatanga”.
“Uhuru amesema kuwa wabunge wote wa Jubilee watahitajika kuunga mkono ajenda za serikali la sivyo wang’atuke,” mbunge mmoja ambaye alihudhuria kikao hicho, lakini akaomba jina lake libanwe, akaambia Taifa Leo.
“Aliwataka wabunge hao kuunga mkono Agenda Nne Kuu za Serikali na kazi ya Kamati ya Maridhiano inayoongozwa na Seneta wa Garissa Yusuf Haji,” akaongeza huku akiongeza kuwa wabunge walitakiwa kuonyesha umoja bungeni.
Rais alimgeukia Bw Tuju na kumwamuru ahakikishe kuwa kamati ya nidhamu ya chama hicho imeimarishwa ili kukabiliana na wabunge waasi.
“Hii, alisema, inajumuisha, kuwafurusha kutoka chama cha kilichowadhamini bungeni,” mwanasiasa huyo alieleza.
Mapema mwezi huu mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri alimshutumu Rais Kenyatta kutokana na hatua yake ya kushirikiana na Bw Odinga akisema hatua hiyo inalenga kuhujumu nafasi ya Bw Ruto kuingia Ikulu.
Naye mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria alionekana kumlaumu Rais Kenyatta kwa kile alichosema ni mwenendo wake wa kupeleka maendeleo kwingineko na kuipa kisogo eneo la Mlima Kenya ambalo lilimpa kura kwa wingi katika uchaguzi mkuu wa 2017.