Habari

Uhuru azidi kumkalia Ruto

May 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

MSIMAMO wa kiongozi wa chama cha Jubilee, Rais Uhuru Kenyatta uliendelea kudhihirika wazi Ijumaa wandani wa Naibu Rais William Ruto wakishindwa kumwokoa Naibu Spika wa Seneti Kithure Kindiki.

Hatua hiyo ilijiri baada ya maseneta wa upinzani kuungana na wale wa Jubilee ambao ingawa walisifia utendakazi wa Profesa Kindiki, walisalimu amri ya chama cha Jubilee.

Chama cha Jubilee kimeendelea kuwatenga wanaoonekana kwenda kinyume na msimamo wa chama hasa wanaoegemea kwa Dkt Ruto, ambaye pia ameendelea kukimya kuhusu yanayoendelea chamani, na kuangazia kutoa msaada kwa waathiriwa wa virusi vya corona.

Baadhi ya maseneta ambao wamekuwa waaminifu kwa Dkt Ruto, hasa maseneta maalum, walilazimika kusaliti imani yao kwake kwa kuunga mkono hoja hiyo iliyowasilishwa na kiranja wa wengi Irungu Kang’ata.

Prof Kindiki ni mwandani wa Dkt Ruto na masaibu yaliyomfika yanasawiriwa kama pigo kwa mustakabali wa kisiasa wa naibu huyo wa Rais katika azma yake ya kuingia Ikulu 2022.

Na licha ya wandani wa Naibu Rais wakiongozwa na Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen kulalamika kuwa hoja hiyo ilikwenda kinyume cha Katiba na Sheria za Bunge, Seneta James Orengo alipuuzilia mbali madai hayo.

“Mheshimiwa Spika wapi orodha ya mashtaka dhidi ya Prof Kindiki? Na je, wapi ushahidi kuonyesha kuwa alipewa nafasi ya kujitetea? Ni udikteta kwa bunge hili kumsulubisha mwenzetu kinyume cha sheria,” Murkomen akasema kwa hasira.

Bw Orengo, ambaye ni kiongozi wa wachache, alisisitiza kuwa kanuni hiyo huzingatiwa katika hoja ya kumfuta kazi Rais na Naibu wake pekee, akisema Kindiki anaondolewa kwa kuwa chama chake hakina tena imani naye.

Kauli yake iliungwa mkono na kiranja wa wachache, Bw Mutula Kilonzo Junior ambaye alisema kosa kubwa la Prof Kindiki ni kutokuwa mwaminifu kwa chama.

“Hoja hii haina uhusiano wowote na utendakazi wa ndugu yangu Prof Kindiki. Suala ni kwamba chama cha Jubilee kilichompa cheo hiki kimekosa imani naye,” akasema Seneta huyo wa Makueni.

Miongoni mwa maseneta waliohudhuria mkutano huo ni wale sita ambao walikwepa mkutano wa awali, ulioitishwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Wao ni Millicent Omanga, Falhada Iman, Naomi Waqo, Victor Prengei, Mary Seneta na Christine Zawadi ambao wameitwa kufika mbele ya kamati ya nidhamu ya Jubilee ili waadhibiwe.

Hata hivyo, licha ya kuhudhuria mkutano huo Seneta Linturi alikataa kuunga mkono hoja hiyo akisema sharti apewe “orodha ya makosa ya Kindiki niyachunguze kwanza kabla ya kufanya uamuzi.”

Mnamo Alhamisi Bw Kang’ata aliwatumia jumbe maseneta wote 38 wa Jubilee wakitakiwa kuhudhuria kikao maalum cha seneti na kuunga mkono hoja ya kumwondoa Kindiki.

Seneta wa Kaunti ya Tharaka Nithi Prof Kithure Kindiki. Picha/ Maktaba

Wale ambao watakosa kuhudhuria kikao hicho wanaweza kupewa adhabu, ambayo inaweza kujumuisha kufurushwa kutoka Jubilee kulingana na kipengee 17 (2) na (3) ya katiba ya chama hicho.

“Msimamo wa chama ni kwamba, kimepoteza imani na Naibu Spika na hivyo kinataka aondolewe. Kwa hivyo, sharti uhudhurie kikao maalum cha seneti na upige kura kulingana na msimamo wa chama,” Bw Kang’ata akasema katika barua yake.

“Tafadhali zingatia kuwa msimamo chama katika suala hili ni kuunga mkono hoja hiyo,” barua hiyo ikaongeza.

Ni kutokana na tishio hilo ambapo wengi wa maseneta waliokuwa katika kambi ya Dkt Ruto walilazimika kubadili msimamo na kuunga mrengo wa Rais.

Upande wa Dkt Ruto uliachwa na idadi ndogo ya maseneta ambao hawawangeweza kubatilisha uamuzi wa kumfurusha Kindiki.

Maseneta waliopiga kura kuunga hoja kutimua Naibu Spika huyo walikuwa 54 dhidi ya 7 waliopinga.