Uhuru kona mbaya kutuliza ghadhabu za Wakenya
Na WAANDISHI WETU
RAIS Uhuru Kenyatta anarejea nchini kutoka China akiwa kwenye kona mbaya kutokana na shinikizo ambazo zimetokana na nyongeza ya asilimia 16 ya VAT kwa bidhaa za mafuta.
Rais atafika nchini akikodolewa macho na Wakenya wanaomtaka kuweka sahihi Mswada uliopitishwa na Bunge kutaka kuahirishwa kwa utekelezaji wa VAT hadi Septemba 1, 2020.
Kwa upande mwingine Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF) liko macho kuona iwapo atapuuza masharti lililowekea Kenya ili kulipa deni linalodia kulipwa sasa la Sh151 bilioni.
Rais Kenyatta anarudi nyumbani akifahamu kuwa wananchi wamekasirika kutokana na ushuru huo ambao umesababisha bei ya petroli kufikia wastani wa Sh130 kwa lita, gharama gesi ya kupikia kwenda juu, nauli kupanda huku bidhaa zingine zikitarajiwa kuwa ghali karibuni.
Pia anaelewa kuwa nyongeza hiyo ni kiboko kwake kisiasa ikizingatiwa shinikizo za kumtaka kusitisha nyongeza hiyo zimetoka hata kutoka kwa wandani wake katika Jubilee.
Mnamo Jumatatu kulishuhudiwa maandamano mjini Nakuru na Narok, huku wasafirishaji mafuta wakigoma Nairobi kulalamikia nyongeza hiyo wanayosema imewaathiri kibiashara. Hatua hiyo ilisababisha uhaba wa mafuta katika baadhi ya vituo vya petroli jijini Nairobi jana.
Wahudumu wa matatu na mabasi nao wameongeza nauli kutokana na ushuru huo, hali ambayo imezua vilio, hasira na malalamiko kutoka kwa wananchi wanaohisi serikali inawanyanyasa kwa kuwabebesha mzigo mzito wa ushuru.
Ushuru huo pia umekosa kuungwa mkono na sehemu kubwa ya wabunge hata katika chama cha Jubilee na pia magavana ambao wametaja nyongeza hiyo ya VAT kama yenye athari mbaya kwa uchumi na maisha ya wananchi wa kawaida.
Viongozi wa upinzani pia wamemshinikiza Rais kutoa uamuzi wa kusimamisha utekelezaji wa nyongeza hiyo.
Lakini iwapo Rais Kenyatta atasikia kilio cha Wakenya na kutia saini kuchelewesha kwa ushuru huo kwa miaka miwili, itambidi atafute njia zingine za kupata pesa za kulipa madeni yanayodaiwa Kenya.
Mojawapo ya njia hizo ni kuongeza ushuru wa VAT kutoka asilimia 16 hadi 18, ili uwe sambamba na wa mataifa mengine ya Afrika Mashariki. Hatua hii pia itaongeza mzigo wa ushuru kwa raia.
Serikali pia inaweza kupunguza migao ya bajeti kwa wizara, hatua ambayo huenda ikatishia utekelezaji wa Ajenda Nne Kuu za Jubilee.
Njia nyingine itakuwa kutafuta mikopo mipya kutoka mataifa ya nje, mbinu ambayo itatumbukiza taifa katika mtego mbaya zaidi wa madeni.
“Iwapo ushuru mpya hautatekelezwa, itahitajika njia nyingine ya kupata fedha kutumika kupitia mikopo au mbinu mpya ya utozaji ushuru ikiwemo kuangalia upya kiwango cha ushuru unaotozwa bidhaa zote kwa lengo la kuupandisha kutoka asilimia 16 hadi asilimia 18 kama mataifa mengine ya Afrika Mashariki,” ikasema taarifa iliyonakiliwa kutoka kwa Hazina ya Kitaifa.
Rais Kenyatta pia hawezi kukataa kulipa madeni anayodaiwa kwani hili linaweza kupelekea Kenya kuwekewa vikwazo vya kiuchumi na IMF, hali inayoweza kuangusha uchumi na hivyo kuzua misukosuko.
Taarifa za JOHN NJIRAINI, WYCLIFFE MUIA na CECIL ODONGO