Uhuru na Raila waomboleza abiria 157 walioangamia Ethiopia
Na CHARLES WASONGA
RAIS Uhuru Kenyatta na kinara wa chama cha ODM Raila Odinga wameongoza Wakenya kuwaomboleza waliofariki katika ajali iliyohusisha ndege ya shirika la ndege la Ethiopian Airline.
Abiria wote 157 waliokuwa kwenye ndege hiyo, miongoni mwao Wakenya 32, walifariki katika ajali hiyo iliyotokea dakika chache baada ya kuanza safari ya kuja Nairobi, Kenya.
Kupitia akaunti zao za Twitter Rais Kenyatta na Bw Odinga walisema wamehuzunishwa na habari kuhusu ajali hiyo huku wakiahidi kushirikiana na familia za wafu hao katika maombi.
“Tumehuzunishwa na habari kwamba ndege ya abiria ya Shirika la Ndege la Ethiopia imeanguka dakika sita baada ya kuanza safari kuelekea Kenya. Natuma risala zangu za rambirambi kwa familia na marafiki ya wale wote waliokuwa katika ndege hiyo,” Rais Kenyatta akasema.
“Natuma rambirambi zangu kwa watu wa Ethiopia kufuatia ajali ya ndege la Shirika la Ndege la Ethiopia. Naombea familia na marafiki ya waathiriwa wote. Kwa Wakenya wenzangu waliopoteza wapendwa katika ajali hiyo, Mungu awape nguvu ya wakati huu wa msiba. Tunashirikiana nanyi katika maombi,” Bw Odinga akasema kupitia Twitter.
Akiongea na wanahabari baada ya ajali hiyo kuripotiwa Waziri wa Uchukuzi Bw James Macharia alithibitisha abiria 32 kati ya waliofariki walikuwa ni Wakenya.
Vile vile, ilisemekana kuwa rubani wa ndege hiyo, Yared Mulugeta ni Mkenya aliyezaliwa nchini Ethiopia. Hii ni kulingana na Afisa Mkuu Mtendaji wa Shirika hilo la ndege la Ethiopia Gebremariam.
Na kulingana na Shirika la Kitaifa la Habari la Ethiopia (FANA) ndege hiyo ilikuwa imebeba abiria kutoka mataifa 34 tofauti.