Ukuaji wa uchumi washuka
Na CHARLES WASONGA
UKUAJI wa uchumi wa Kenya ulipungua hadi asilimia 5.4 mwaka 2019 kutoka asilimia 6.3 mnamo 2018, takwimu za hivi punde zinaonyesha.
Hali hali itakuwa mbaya zaidi mwaka 2020 kutokana na janga la corona huku ikikadiriwa kuwa kiwango hicho kitashuka hadi asilimia 3.2 jinsi alivyoeleza Waziri wa Fedha Ukur Yatani.
Kulingana na data kutoka Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) sekta zote za uchumi ziliandikisha kushuka kwa kiwango cha ukuaji.
Kwa mfano, mapato kutokana na sekta ya kilimo yalishuka hadi asilimia 3.6 kutoka asilimia sita mwaka wa 2018.
Hii ni kutokana na hali kwamba kipindi kirefu cha uhaba wa mvua kilivuruga msimu wa upanzi katika maeneo kadha nchini yanayotegemea kilimo.
Ukuaji katika sekta ya uzalishaji bidhaa nao ulififia hadi kiwango cha asilimilia 3.2 kutoka asilimia 4.3 huku sekta hiyo ikiathirika na uhaba wa malighafi
“Hali hii ya kupungua kwa ukuaji ilishuhudiwa katika sekta zote za uchumi, zilizoathirika zaidi zikiwa ni zile za utoaji huduma,” waziri Yatani akasema Jumanne alipotoa ripoti kuhusu hali ya uchumi.
Hata hivyo, Bw Yatani amesema sekta za Fedha na Bima ziliandikisha kuimarika kwa ukuaji hadi asilimia 6.6 mnamo 2019 kutoka asilimia 5.3 mnamo 2018.
Vilevile, uchumi ulizalisha nafasi 846,300 za ajira katika kipindi hicho japo sekta ya umma ilizalisha nafasi chache za ajiri ikilinganishwa na sekta binafsi.
Nafasi za kazi katika sekta ya umma ilipungua kwa kiasi cha nafasi 67,800.
Sekta ya juakali iliendelea kutoa nafasi nyingi za ajira kwa kuongeza nafasi 767,900 mwaka 2019 kutoka nafasi 744,100 mnamo 2018.
Mnamo 2019 Utajiri Jumla wa Kitaifa (GDP) ulikuwa Sh9.74 trilioni.