HabariSiasa

Ulikuwa uamuzi mchungu sana kukutana na Uhuru – Raila Odinga

March 16th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na RUTH MBULA na BARACK ODUOR

Kwa ufupi:

  • Raila asema haikuwa rahisi kwake kukubali kuketi pamoja na Rais Kenyatta na kutia saini mkataba wa maelewano
  • Tangu Agosti 2017, zaidi ya watu 360 wamefariki, hatuwezi kuruhusu hali hii kuendelea nchini, Canaan ni ya kila Mkenya, akasema Bw Odinga
  • Asema sasa atakuwa akirejelewa kama “His Excellency” ambayo ni hadhi ya Rais wala sio “Right Honorable” ambayo ni hadhi ya Waziri Mkuu
  • Pamoja na Rais Kenyatta, watafanya ziara kote nchini kuwafafanulia wananchi mengi kuhusu ushirikiano wao

KIONGOZI wa upinzani, Raila Odinga, Ijumaa alisema uamuzi wake wa kukutana na Rais Uhuru Kenyatta ulikuwa mchungu lakini utawafaa mamilioni ya Wakenya.

Kulingana na Bw Odinga, haikuwa rahisi kwake kukubali kuketi pamoja na Rais Kenyatta na kutia saini mkataba wa maelewano (MOU).

Lakini alifafanua kuwa mwafaka huo haumaanishi kuwa amejiunga na Jubilee akisema NASA ingali imara licha ya malalamishi yaliyoibuliwa na vinara wenzake.

“Nimesikia kuna watu ambao wana wasiwasi kuhusu umoja ndani ya NASA. NASA ni NASA. Na Jubilee ni Jubilee. Tuko tofauti. Muungano wetu ni imara licha ya tofauti za kimawazo za hapa na pale,” akasema.

Akiongea katika kaunti za Kisii na Homa Bay kwa mara ya kwanza tangu mkutano huo, Bw Odinga alisema yuko tayari kushirikiana na Rais Kenyatta kwa manufaa ya maelfu ya Wakenya waliokufa katika ghasia za uchaguzi miaka kadha iliyopita.

 

Vifo 360

“Huu ulikuwa uamuzi mchungu zaidi. Tumeshuhudia umwagikaji wa damu sehemu mbalimbali nchini tangu 1992. Na tangu Agosti 2017, zaidi ya watu 360 wamefariki, hatuwezi kuruhusu hali hii kuendelea nchini,” akasema Bw Odinga.

Alisikitika kuwa Kenya imegawanywa kwa misingi ya kikabila ambapo watu wanatambuliwa kwa majina yao wala sio thamani, na majina ndiyo humwezesha mtu kupata au kupoteza kazi.

“Tulikubaliana kwamba, sharti kujenga taifa moja lenye amani. Hii ndio maana nilikubali kuketi na Rais Uhuru kwa niaba ya mamilioni ya Wakenya ambao ninawakilisha.”

“Ilinilazimu kumtazama machoni na kumwambia kwamba, sharti tukomesha dhuluma za kihistoria. Ndiposa tukaita makubaliano yetu ‘Building Bridges’ (Kujenga Madaraja),” akasema.

Bw Odinga alisema MoU yao inaangazia masuala ya ushirikishaji wa wote, kuangamiza umasikini, ufisadi, kuimarisha usalama, kati ya mengine.

“Tukikubaliana kuhusu masuala haya yote tutajenga Kenya nzuri kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Tunaweza kuafikia haya tukikubali kufanyakazi pamoja.

Alisema hayo alipowahutubia viongozi wa kaunti ya Kisii wakiongozwa na Gavana James Ongwae, kabla ya kuhudhuria hafla ya mazishi ya Profesa Tumbo Oeri.

 

Canaan ni ya kila Mkenya

“Makabila yote 44 nchini sharti yatembee pamoja kwenda Canaan,” akasema akitumia neno “Canaan” kuashiria maisha mazuri.

Waziri huyo Mkuu wa zamani alisema sasa atakuwa akirejelewa kama “His Excellency” ambayo ni hadhi ya Rais wala sio “Right Honorable” ambayo ni hadhi ya Waziri Mkuu.

Alisema mgawanyiko wa kisiasa ambao umekuwepo nchini tangu uhuru ilifikia kikomo aliposalimiana na Rais Kenyatta.

Bw Odinga alieleza kuwa yeye na Rais hawakusema mengi kuhusu mwafaka wao kwani walitaka kupata hisia za Wakenya kabla ya kutoa maelezo kamili.

“Tulitaka Wakenya kujadili wazo hili kwa undani kwanza kabla ya kutoa mwelekeo kuhusu jinsi ambavyo malengo yake yatafaulishwa.

 

Ziara kote nchini

Wakati huo huo, Bw Odinga ambaye ni kiongozi wa ODM aliwaambia wakazi wa kaunti ya Kisii kwamba, pamoja na Rais Kenyatta, watafanya ziara kote nchini kuwafafanulia wananchi mengi kuhusu ushirikiano wao.

Gavana Ongwae ambaye alimpokea Bw Odinga aliunga mkono ushirikiano wake na Rais Kenyatta, akisema ndio njia ya kipekee kuwezesha Kenya kutimiza ndoto yake.

Naye Seneta wa Kisii, Prof Sam Ongeri alisema mkutano kati ya viongozi hao wawili ulikuwa ishara tosha kwamba wao ni wazalendo.

“Wale wanaopiga kelele hatimaye watarudi kwa Raila kwa sababu mkutano wao ulijibu maombi ya Wakenya wengi. Sawa na Joshua na Musa, Raila na Uhuru ndio wenye ufunguo wa fanaka kwa taifa hili,” akasema Profesa Ongeri.