Habari

Ushindi kwa Uhuru akitajwa kiongozi halali wa Jubilee baada ya jaribio la chama kutekwa

Na BENSON MATHEKA July 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS mstaafu Uhuru Kenyatta amepata ushindi mkubwa baada ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) kumthibitisha kuwa kiongozi halali wa chama cha Jubilee.

Hatua hii imemrejesha rasmi kama kiongozi wa chama hicho alichotumia kuchaguliwa kwa muhula wa pili kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu ulioidhinisha maamuzi ya Mkutano Mkuu Kitaifa wa Wajumbe uliozua mzozo.

Hatua hiyo imekomesha mgogoro wa muda mrefu wa uongozi uliogawanya chama hicho baada ya kundi pinzani lililoongozwa na mbunge maalum, Bi Sabina Chege na mwenzake wa Bunge la Afrika Mashariki, Bw Kanini Kega, kudai kuwa wao ndio viongozi halali wa Jubilee.

Mvutano huo ulianza baada ya kundi hilo kujaribu kuwaondoa washirika wa Bw Kenyatta kwa madai kwamba waliondolewa kwa mujibu wa taratibu za ndani za chama.

Bi Chege alijitawaza kiongozi wa chama huku Bw Kega akishikilia wadhifa wa Katibu Mkuu. Wawili hao walifanya mapinduzi ya uongozi katika Jubilee, wakidai Rais mstaafu hawezi kushiriki shughuli za chama.

Hata hivyo, Mahakama Kuu ilitambua maamuzi ya Mkutano Mkuu wa Kitaifa wa Wajumbe (NDC) uliofanyika Mei 2023, ambapo Bw Kenyatta alirejeshwa rasmi kama kiongozi wa chama.

Miongoni mwa viongozi waliothibitishwa katika mabadiliko hayo mapya ni Bw Saitoti Torome, ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Kitaifa, akichukua nafasi ya Bw Nelson Dzuya, huku Bw Jeremiah Kioni akidumishwa kama Katibu Mkuu.

Bw David Murathe ameendelea kuwa Naibu Mwenyekiti wa Kitaifa, huku viongozi wengine wapya kama Bi Beatrice Gambo, Bw Joseph Manje, Bw Yassin Noor, na Bw Kados Muiruri wakichukua nyadhifa mbalimbali za juu chamani.

Wakati huo huo, viongozi waliokuwa katika mrengo pinzani kama Bw Kega, Bi Naomi Shaban, na Bw Joshua Kutuny, waliondolewa katika nyadhifa zao, hatua inayoashiria kuimarika kwa udhibiti wa Bw Kenyatta katika chama hicho.

Uamuzi huu wa mahakama na hatua ya ORPP umepatia Jubilee uthabiti kisheria, jambo linalowezesha chama kushiriki shughuli za kisiasa na kuwasiliana na mashirika kama Tume ya IEBC kwa mujibu wa sheria.

Pia, hatua hiyo inapatia Jubilee haki ya kupokea ufadhili wa chama kutoka kwa serikali.

Mabadiliko haya yanajiri wakati chama hicho kinapanga kumtangaza Dkt Fred Matiang’i, aliyekuwa Waziri katika serikali ya Bw Kenyatta, kama mgombea wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2027.

Inasemekana Dkt Matiang’i anaungwa mkono na Bw Kenyatta, na anatarajiwa kuwa mmoja wa wapinzani wakuu wa Rais William Ruto katika kinyang’anyiro hicho.

Kwa mara nyingine, Bw Kenyatta ameonyesha kuwa bado ana ushawishi mkubwa katika siasa za kitaifa, huku akilenga kuunda upya muungano wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu ujao.