Habari

Ushoga waeneza Ukimwi magerezani

August 15th, 2019 2 min read

MARY WANGARI Na ANGELA OKETCH

IDADI kubwa ya wafungwa katika magereza ya Kenya wameambukizwa Ukimwi kutokana na kuongezeka kwa visa vya ushoga.

Kulingana na utafiti uliofanywa na shirika la Resources Oriented Development Initiative Kenya, katika kila wafungwa 10, wapatao sita wana virusi vya HIV, hii ikiwa ni asilimia 56 ya wafungwa wote.

Kwa kawaida wafungwa wanapopelekwa gerezani kwa mara ya kwanza hufanyiwa vipimo vya virusi vya HIV, homa ya ini pamoja na kifua kikuu. Hata hivyo, wengi wanaoingia bila HIV hupatikana wameambukizwa miezi michache tu baada ya kuanza kifungo.

Uchunguzi huo uligundua kuwa wafungwa wengi hasa wale wapya huwa wanabakwa huku wengine wakikubali kushiriki ushoga kutoka na hali ngumu gerezani.

Pia magereza huwa yanashuhudia visa vingi vya ghasia zinazotokana na mizozo ya kupigania watu wa kushiriki nao ushoga.

Kinachochangia zaidi maambukizi ya HIV ni kuwa wafungwa hawana namna ya kujikinga kutokana na maambukizi kwa kuwa kondomu ni marufuku gerezani.

“Ikifanikiwa kupitishwa hadi gerezani, pakiti ya kondomu, ambayo kwa kawaida huuzwa kwa Sh40, huuzwa kwa Sh200 gerezani,” alisema mfungwa mmoja kutoka Kakamega.

Kulingana na mfungwa mwingine aliyekataa kutambulishwa, siku ya kwanza gerezani ndiyo jinamizi kuu kwa kila mfungwa: “Wafungwa wapya huuzwa kama bidhaa mnandani, ambapo mfungwa anayetoa kiasi kikubwa zaidi cha pesa hujitwalia ‘mke’ mpya. Wanaopendwa sana ni wafungwa ambao ni mara yao ya kwanza kuwa gerezani.”

Wafungwa wachanga nao hulazimishwa kushiriki ushoga ili wanufaike na chakula, malazi bora au hata kupiga simu ya kuwajulia hali jamaa nyumbani.

“Wafungwa wanaowavizia wale wachanga hujifanya wakarimu. Kwa kawaida seli huwa zimejaa lakini ‘mumeo’ atakuruhusu ulale kwenye godoro lake, ushiriki chakula chake lakini inapofika usiku ni lazima utalipa gharama,” anasema mfungwa.

Uhaba wa vifaa vya kimsingi kama vile vyoo, bafu, godoro na karatasi za msalani pia umechangia kuongezeka kwa ushoga.

Hata hivyo, licha ya ushoga kukithiri katika magereza, wahusika hufanya tendo hilo kwa siri ili kuepuka adhabu wanapopatikana na askari wa magereza.

“Adhabu inakuwa ni kutengwa, kulazimishwa kulala sakafuni na kupunguziwa mgao wa chakula,” akasema mfungwa.

Bw Alphonse Simon, ambaye ni mwelekezi wa kudhibiti Ukimwi katika magereza ya Kenya alithibitisha kuwepo kwa ushoga katika jela za Kenya ambao hufanywa kisiri huku akisema wahusika wanafahamu vyema wakipatikana wataadhibiwa vikali.

Mnamo Mei mwaka huu, Mahakama Kuu nchini Kenya iliharamisha ushoga ambapo adhabu yake kisheria ni miaka 14 gerezani.

Mnamo 2002, ombi mojawapo lililowasilishwa na wafungwa katika gereza la Industrial Area lilikuwa kuitaka sheria kutambua haki zao kushiriki tendo la ndoa.

Wafungwa pia walimwomba serikali kuwaruhusu wanandoa kushiriki kushiriki ngono katika maeneo yaliyotengwa gerezani ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya Ukimwi na ushoga gerezani.