HabariSiasa

Usijaribu kumruka Ruto, Uhuru aonywa

December 19th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na ONYANGO K’ONYANGO

KUNDI la viongozi kutoka Rift Valley Jumanne lilionya kuwa halitaruhusu Rais Uhuru Kenyatta kumhujumu naibu wake William Ruto.

Viongozi hao, wakiongozwa na Mbunge wa Soy Caleb Kositany pia walisema, hawataruhusu kinara wa ODM Raila Odinga kuchukua nafasi ya Bw Ruto katika serikali ya Jubilee.

Walisema hawatakubali Rais Kenyatta kugawana mamlaka na Bw Odinga huku wakimtaka kiongozi wa nchi kukumbuka historia ya chama cha Jubilee.

“Tunaunga mkono yanayofanywa na Rais Kenyatta, ikiwemo vita dhidi ya ufisadi. Lakini hatutakubali kugawana mamlaka na Bw Odinga aliyejiunga nasi baada ya kusalimiana na rais,” akasema Bw Kositany.

Mbunge huyo aliungwa mkono na wenzake Seneta wa Nandi Samson Cherargei na mbunge wa Keiyo Kusini Daniel Rono ambao walionya Bw Odinga dhidi ya kujaribu kumwondoa Bw Ruto serikalini.

“Tulipigana na tukashinda uchaguzi; hivyo hatuwezi kuwa sawa na wapinzani wetu ambao wamekubali kushirikiana nasi,” akasema Bw Rono.?Bw Cherargei alionya kuwa wabunge wa mrengo wa Bw Ruto hawataruhusu ugavi sawa wa mamlaka na rasilimali na Bw Odinga.

“Watu hawafai kudanganyika kwamba kuna ugavi sawa wa mamlaka baina ya Jubilee na Bw Odinga,” akasema seneta huyo katika mahojiano ya simu na Taifa Leo.?Lakini Katibu Mkuu wa Kanu Nick Salat na mbunge wa Cherang’any Joshua Kutuny waliwashutumu viongozi hao na kuwataka kukoma kuendeleza siasa za migawanyiko ya kikabila.

Bw Kutuny alionya kuwa hatua ya wandani wa Bw Ruto kuendelea kumshambulia Bw Odinga kila wanaposimama kwenye jukwaa la kisiasa itampatia umaarufu mkubwa kiongozi wa Upinzani.

“Viongozi hawa wanafaa kuelewa kuwa Bw Odinga ndiye anatamba katika ulingo wa siasa kwa sasa hivyo kupigana naye kunamfanya kuwa maarufu na mwenye ushawishi zaidi. Vilevile, wanaendelea kuthibitishia Wakenya kuwa wanaendeleza siasa za kuleta mgawanyiko wa kisiasa,” akasema Bw Kutuny.

Bw Salat alimtaka rais kuhakikisha rasilimali zinagawanywa kwa usawa katika maeneo yote ya nchi.

“Kenya haifai kuwa nchi ambapo watu wanachinjana kila baada ya miaka mitano. Ili kukomesha hali hii, tunafaa kukumbatia muafaka baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga na kuhakikisha kila eneo linanufaika na miradi ya maendeleo,” akasema Bw Salat.?Rais Kenyatta alipokuwa akizungumza jijini Kisumu Alhamisi iliyopita, alisema Bw Odinga yuko ndani ya serikali, kauli ambayo inaonekana kuwakera wandani wa Bw Ruto.

Rais Kenyatta pia alisema kuna haja ya kukomesha uhasama wa kikabila ambao hujitokeza kila baada ya uchaguzi mkuu.

“Tunafaa kuangalia kwa makini hili suala ambapo mshindi wa uchaguzi anachukua kila kitu huku waliopoteza wakiambulia patupu,” akasema Rais Kenyatta.

Kauli hiyo ya rais imeibua tetesi kuwa huenda anaunga mageuzi ya katiba kupitia kura ya maoni.