Habari

Utaenda jela ukikataa sensa

August 23rd, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

WAKENYA watakaosusia shughuli ya kuhesabu watu itakayoanza Jumamosi jioni, wanakabiliwa na hatari ya kutozwa faini ya Sh500,000 ama kufungwa jela mwaka mmoja au adhabu zote mbili.

Kulingana na sheria, ni hatia kukataa kushiriki shughuli hiyo ya kitaifa ya kukusanya takwimu, kuharibu au kuvuruga utaratibu huo.

Baadhi ya Wakenya wametisha kususia shughuli hiyo wakisema uteuzi wa maafisa watakaoiendesha haukuwa wa haki.

Walioapa kususia shughuli hiyo wanasema watu kutoka maeneo yao walibaguliwa wakati wa kuajiri maafisa wa kuendesha shughuli hiyo.

Kulingana na Sheria ya Takwimu iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019, adhabu ya kuzuia maafisa wa sensa na kutoa habari za uwongo ni faini ya Sh500,000.

Kulingana na sheria hiyo, watu watakaokataa kujibu maswali ya maafisa watakaoendesha sensa au kutoa habari za kupotosha watatozwa faini au kufungwa jela miezi sita.

“Yeyote ambaye kwa makusudi, anakataa kutoa habari inavyohitajika anavunja sheria na akipatikana na hatia atatozwa faini isiyozidi Sh500,000, kufungwa jela miezi sita au hukumu zote mbili,” inaeleza sheria hiyo.

Kabla ya sheria kufanyiwa marekebisho, adhabu ya kususia na kudanganya katika sensa ilikuwa Sh100,000 au kufungwa jela mwaka mmoja.

Tayari, serikali imeagiza Wakenya kukaa nyumbani kuanzia Jumamosi jioni hadi Jumapili ili waweze kuhesabiwa.

Itakuwa mara ya kwanza shughuli hiyo kuendeshwa kwa kutumia mitambo ya kidijitali, hatua ambayo serikali inasema itahakikisha habari zitakuwa sahihi na zinaweza kupatikana haraka.

Kila Mkenya atahesabiwa mahali atakuwa na serikali imeonya wanasiasa wanaopanga kusafirisha watu hadi maeneo yao kushiriki sensa.

“Tumepokea ripoti kwamba baadhi ya wanasiasa walifanya mikutano kupanga kusafirisha watu hadi kaunti zao. Hii ni tabia duni inayopaswa kukoma. Tunawatazama na mtakabiliwa na mkono wa sheria,” alionya Bw Matiang’i kwenye kikao cha wanahabari akiandamana na kaimu Waziri wa Fedha, Ukur Yatani na mwenzao wa Habari na Teknolojia Joe Mucheru.

Wanasiasa wakiwemo wabunge na magavana wamekuwa wakihimiza raia kurudi maeneo walikozaliwa kuhesabiwa huko.

Hii ni kutokana na haja ya kuwa na idadi kubwa ya watu kwa ajili ya ugawaji wa pesa mashinani pamoja na mipaka ya maeneobunge.

Mawaziri hao walisema maandalizi ya sensa yamekamilika na wakahakikishia Wakenya kwamba usalama wao umelindwa. Baadhi ya maswali ambayo Wakenya watatakiwa kujibu ni kuhusu umri, jinsia, dini, jamii, eneo la kuzaliwa, elimu na kazi.

Wakenya pia wataulizwa kuhusu mali waliyo nayo ikiwemo mifugo na vifaa vya nyumbani.

Watu wote watakaokuwa nchini kuanzia Jumamosi saa kumi na mbili jioni watahesabiwa.

Serikali yaweka mikakati

Serikali imesema imeweka mikakati ya kuhesabu watu watakaokuwa wakisafiri, watakaokuwa kwenye mahoteli na lojing’i, wagonjwa watakaokuwa hospitalini na wafungwa wote magerezani Jumamosi usiku.

Maafisa wa kuhesabu watu watakuwa wakiandamana na wazee wa vijiji ili watambuliwe kwa urahisi.

Mtu akikosa kuhesabiwa Jumamosi usiku atahesabiwa kwa kurejelea mahali akakuwa usiku wa Agosti 24/25.

Shughuli hii itaendelea hadi Agosti 31 na serikali inasema itatoa nambari ya simu ya kupiga bila malipo ili wale ambao watakosa kusajiliwa katika muda huo wawasiliane na KNBS.

Shirika hilo litatuma maafisa kuhesabu watu hao nyumbani kwao.