HabariSiasa

Vigogo wa Ruto kichinjioni

June 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

HARAKATI za kuwaondoa wandani wa Naibu Rais William Ruto katika nyadhifa mbalimbali bungeni zinatarajiwa kufikia kilele wiki hii huku shoka likielekezwa kwa wabunge Aden Duale na Caleb Kositany.

Hatua ya kuwang’oa wawili hao katika nyadhifa mbalimbali inajiri baada ya wabunge wapatao 130 wa Jubilee kutia sahihi hoja ya kumng’oa Bw Duale katika wadhifa wake kama Kiongozi wa Wengi bungeni, huku Bw Kositany akitazamiwa kuvuliwa mamlaka kama Naibu Katibu Mkuu wa Jubilee kufuatia hatua ya mrengo wa Tangatanga kutoa ishara za kuunda chama mbadala cha Jubilee Asili. Bw Kositany ni mtetezi sugu wa Dkt Ruto.

Harakati hizo za kung’oa ‘mizizi’ ya Dkt Ruto kutoka serikali ya Rais Kenyatta zinaonekana kulenga kumtenga ili abakie bila ushawishi wowote mbali na kumshinikiza hadi ama ajiondoe serikalini au awe mdhaifu kiasi cha kung’atuliwa kwa urahisi.

Kilele cha harakati hizo kinatarajiwa kuwa kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa, kati ya vyama rafiki, ambayo itatoa mwelekeo kuhusu uchaguzi mkuu wa 2022. Hali hii itamaanisha kuwa Rais Kenyatta atakuwa amekiuka ahadi yake ya mwaka 2013 ya kumuunga mkono naibu wake kurithi Ikulu.

Kwa mujibu wa Naibu mwenyekiti wa Jubilee, Bw David Murathe, hatua madhubuti zitachukuliwa kuwang’oa washirika wa Dkt Ruto kutoka nyadhifa zote ndani ya chama na pia ndani ya serikali “tukianza na Duale wiki ijayo na hatimaye kuiosha serikali yote ‘uchafu’ wa washirika wa Naibu Rais”.

Alisema kuwa naye Bw Kositany, akiwa mbunge wa Soy, atang’olewa kama naibu wa katibu mkuu wa Jubilee kwa kuwa ameenda kinyume na katiba ya chama ambapo amefungua afisi mbadala za chama cha Jubilee na kutangaza kuwa hana imani na maafisa wenzake.

“Kositany ni mfuasi wa chama kipya kinachoitwa Jubilee Asili. Yeye sasa ni afisa katika chama hicho na hawezi akawa afisa katika vyama viwili vya kisiasa,” akasema Bw Murathe ambaye ni mwandani wa Rais Kenyatta.

Alisema kuwa zaidi ya sahihi 100 kati ya wabunge wote 179 wa Jubilee zimewekwa kupendekeza Bw Duale ang’olewe, mchakato ambao tayari Rais kama kiongozi wa chama amefahamishwa.

“Kabla ya wiki ya kuamkia kesho kutamatika, Duale atakuwa ameondolewa katika wadhifa wake. Kwa sasa, Duale ni kigae tu katika wadhifa huo kwa kuwa amepokonywa majukumu muhimu aliyokuwa nayo na ambayo tayari yamekabidhiwa mbunge wa Kipipiri, Bw Amos Kimunya ambaye kwa sasa ndiye daraja la wabunge wa Jubilee na Ikulu,” akasema.

Mbunge wa Kieni, Bw Kanini Kega alisema kuwa yeye ndiye anayeongoza harakati hizo za kumng’oa Bw Duale akisema, “Huyu (Duale) ni mfuasi sugu wa mrengo ambao hauna heshima kwa Rais Uhuru na sera zake za kiuchumi na kisiasa.”

Bw Kega alisema kuwa Rais ndiye aliyetoa idhini kwa wabunge wa Jubilee kutafakari kuhusu ufaafu wa Duale na ikiwa anatosha kuendelea mbele na majukumu yake, asalie na ikiwa hatoshi, atimuliwe.

“Wengi wetu wameafikiana kuwa hatoshi na ndipo katika mkutano wa wabunge wa Jubilee katika Ikulu Jumatatu au Jumanne, tutaenda kumng’oa,” akasema.

Hata hivyo, Bw Duale aliambia Taifa Jumapili, “Hakuna wadhifa ambao umeumbiwa mtu fulani kuushikilia daima bali zote huwaniwa na kushikiliwa kwa muda tu.”

Alisema hataki kiujiingiza katika sarakasi za kujibizana kisiasa na wanaoeneza habari za kung’atuliwa kwake akisisitiza kuwa “hata wadhifa wa urais si wake milele bali huwa ni wa awamu tu na wakati utafika hata naye aende nyumbani… Wadhifa wangu uko katika msingi sawa”.

Naye Bw Kositany alisema, “Mimi sijalishwi na matukio yoyote ya sasa ndani ya chama cha Jubilee wala hizi si habari mpya kuhusu kulengwa kwangu na niko tayari.”