Vikosi maalumu vya usalama sasa vyageukia uhalifu
GARI aina ya Subaru Jeusi liliandama gari la Toyota Harrier lililokuwa likitumiwa na mfanyabiashara mmoja Oktoba 19, 2025, hadi karibu na Barabara ya Mirema, Kaunti ya Nairobi.
Ingawa mfanyabiashara huyo alitambua Subaru yenye nambari za kigeni, hakuhisi hatari yoyote hadi wanaume watatu waliporuka kutoka ndani, mmoja akiwa ameshika bunduki aina ya AK-47.
Taifa Leo Dijitali imeamua kutotaja jina la mfanyabiashara huyo kwa sababu za kiusalama na kisheria.
Wanaume hao walimwamuru afungue mlango wa gari lake na kuwapa pesa pamoja na nyaraka zilizokuwa kwenye kiti cha mbele cha abiria.
Walihesabu dola 16,000 za Amerika (sawa na Sh2.06 milioni) na Sh500,000 za Kenya, kisha wakamfungia mfanyabiashara huyo kwenye buti ya Subaru na kuondoka kuelekea Barabara ya Lumumba, eneo la Roysambu.
Baada ya kutolewa garini karibu na Hospitali ya Jessekay, mfanyabiashara huyo alipanda boda boda hadi Kituo cha Polisi cha Kasarani ambapo aliripoti tukio hilo, na uchunguzi ukaanza mara moja.
Uchunguzi ulisababisha kukamatwa kwa wanaume watatu – wawili wakiwa ni maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), kutoka Kitengo Maalum cha Operesheni (OSU), kilichoanzishwa mwaka 2022 kushughulikia uhalifu sugu unaotishia usalama wa taifa.
Mtuhumiwa wa tatu ni afisa wa zamani wa polisi aliyehusishwa na matukio kadhaa ya uhalifu kwa miaka mingi.
Polisi walivamia nyumba moja Kitengela walikopata nambari za usajili za magari, simu saba za mkononi, mkebe wa gesi ya kutoza machozi, vitambulisho, na pingu zilizodaiwa kutumika kukamata watu kinyume cha sheria na kuwatisha wahasiriwa.
Katika msako huo, afisa mwingine wa zamani pia alikamatwa, na baadaye maafisa wengine wawili wa OSU walikamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Majina ya waliokamatwa hayakutajwa kwa sababu za kisheria.
Uchunguzi unaonyesha kuwa tukio la Mirema lilitekelezwa kwa kutumia gari rasmi la DCI, ikionyesha kwamba baadhi ya maafisa wanaotakiwa kulinda raia wamegeuka tishio.
Msemaji wa Polisi, Muchiri Nyaga, alisema tukio hilo ni “kisa cha kipekee ambacho hakipaswi kuhusisha idara nzima.”
Tukio hili limefufua kumbukumbu za vikosi maalum vilivyotangulia nchini, ambavyo vilihusishwa na mauaji ya kiholela, mateso, na vitendo vya kisiasa.
Mtaalamu wa usalama Patrick Shiundu asema umma haujaelewa vyema majukumu ya vikosi maalum vya polisi.
“Hivi vikosi ndivyo vinavyofanya kazi iwe ngumu zaidi katika idara ya polisi,” alisema Shiundu.
Hata hivyo, mwanaharakati wa haki za binadamu Njoki Wamai asema vikosi maalum ni “vikosi vya mauaji” vinavyotisha wananchi na kukiuka haki zao, na hivyo vinapaswa kuvunjwa kabisa.
Kitengo cha OSU kilianzishwa baada ya Rais William Ruto kuvunja Special Service Unit (SSU) mwaka 2022, kilichohusishwa na mauaji ya kiholela ya baadhi ya watu waliokuwa wahusika wa kampeni za kisiasa.
Historia inaonyesha kuwa vikosi maalum vilivyotangulia kama Kanga Squad na Kwekwe Squad vilihusishwa na mauaji, mateso, na utekaji nyara, hali iliyosababisha umma kuonya dhidi ya makosa ya kihistoria yanayoweza kurudiwa.
