Vinara wa NASA wakubaliana kuepuka siasa za 2022
Na VALENTINE OBARA
Kwa ufupi:
- Kwa kauli moja, wamewataka wanachama wao wakomeshe mijadala ya uchaguzi wa 2022 na badala yake, wawe na lengo moja la kupigania haki ya uchaguzi
- Pingamizi zimekuwepo ndani ya NASA katika siku za hivi majuzi kwani inaaminika Bw Odinga ananuia kugombea urais tena 2022
- Wanne hao wamesema wanashuku Jubilee ina nia fiche kuhusu Mswada wa Kamket Kassait
- Wasema wamejitolea kushauriana na serikali ya Jubilee
VINARA wa Muungano wa NASA sasa wamekubaliana kusitisha mijadala kuhusu uchaguzi wa mwaka wa 2022 ambayo imekuwa ikitishia kuwagawanya.
Kumekuwa na mvutano kati ya viongozi wa vyama tanzu vya muungano huo kwa muda sasa kwani kila upande unataka kinara wake awe mgombeaji urais katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanywa 2022.
Vyama vya Wiper, Ford Kenya na Amani National Congress (ANC) vimekuwa vikionekana kukosa hamu ya kuendeleza juhudi za kutetea utendaji wa haki uchaguzini, tofauti na Chama cha ODM ambacho kimekuwa kikisisitiza lazima marekebisho yafanywe kwenye mfumo wa kusimamia uchaguzi kabla watu wazungumzie 2022.
Vinara Raila Odinga (ODM), Kalonzo Musyoka (Wiper), Moses Wetang’ula (Ford Kenya) na Musalia Mudavadi (ANC), kwa kauli moja Jumanne walitaka wanachama wao wakomeshe mijadala ya uchaguzi huo ujao na badala yake, wawe na lengo moja la kupigania haki ya uchaguzi.
“NASA inashikilia msimamo wake kwamba uchaguzi hauwezi kufanywa 2022 kama vyanzo vya ukiukaji wa sheria ulioshuhudiwa 2017 havitatambuliwa kikamilifu na kutatuliwa,” wakasema kwenye taarifa ya pamoja baada ya kukutana jana asubuhi.
Muungano huo ulisusia uchaguzi wa marudio wa urais uliofanywa Oktoba 26, mwaka uliopita kwa kudai kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) haikufanya marekebisho jinsi ilivyoagizwa na Mahakama ya Juu wakati ilipofutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa Agosti 8 ambapo Rais Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi.
Pingamizi zimekuwepo ndani ya NASA katika siku za hivi majuzi kwani inaaminika Bw Odinga ananuia kugombea urais tena katika uchaguzi ujao ilhali inasemekana kulikuwa na maelewano kwamba atamuunga mkono kinara mwingine.
IEBC haiaminiki
Mbali na hayo, vinara walisema pia kuwa IEBC haiwezi kuruhusiwa kusimamia shughuli ya kubadilisha mipaka ya maeneo ya nchi kutokana na yale yaliyotokea mwaka uliopita.
Kuhusu mswada uliowasilishwa na Mbunge wa Tiaty, Bw Kassait Kamket, ambao umependekeza mabadiliko ya mfumo wa uongozi ikiwemo kubuniwa kwa nafasi ya Waziri Mkuu mwenye mamlaka makubwa kuliko rais, wanne hao walisema wanashuku Jubilee ina nia fiche ingawa wanaendelea kuuchanganua.
“Muungano huu utaitisha mkutano wa wabunge wake wote hivi karibuni kutilia mkazo misimamo hii hasa kuhusu suala la haki ya uchaguzi,” wakasema vinara hao.
Hata hivyo, walirejelea kuwa bado wamejitolea kushauriana na serikali kama Jubilee itakubali mojawapo ya ajenda kwenye mashauriano hayo ihusu utendaji wa haki uchaguzini.
Walisema wanatambua kuwa kuna changamoto zingine zinazokumba wananchi ikiwemo uhaba wa chakula, mikopo mikubwa ya taifa na ukabila lakini haki ya uchaguzi ni muhimu kuhakikisha kuna uthabiti wa nchi katika miaka ijayo.