Habari

Wafanyabiashara wawatunuka wateja wao nguo za bure sherehe za Eid al-Fitr

May 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na KALUME KAZUNGU

WAFANYABIASHARA wa mitumba katika mji wa kale wa Lamu wamewatunuka wateja wao nguo za bure wakati wakiadhimisha sherehe za Eid al-Fitr.

Taifa Leo imeshuhudia wateja wakimiminika kwa wingi katika soko la Uwanja wa Kibaki mjini Lamu ili kujichukulia msaada huo wa nguo.

Wafanyabiashara wamekuwa wakitekeleza shughuli hiyo ya kupeana nguo za bure kwa wateja, ambapo wanaolengwa hasa huwa ni wale kutoka jamii za kipato cha chini.

Msemaji wa wafanyabiashara wa mitumba eneo la Lamu, James Babzii, amesema si mara ya kwanza kwao kuwatunuka wateja wao mitumba ya bure ili kuwasaidia wakati huu wa Eid al-Fitr.

“Kila mwaka sisi huwapa wateja wetu nguo za bure hasa kila kipindi cha Idd kinapowadia; hulipi chochote hapa,” amesema Bw Babzii.

Samuel Otieno ambaye ni mmoja wa wafanyabiashara wa mitumba amesema wiki ya mwisho ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kulishuhudiwa wateja wengi wakimiminika vibandani na madukani kujinunulia nguo na bidhaa nyingine tayari kwa maadhimisho ya Eid al-Fitr.

Bw Otieno amesema hatua hiyo ilinogesha vilivyo biashara, licha ya wafanyabiashara wengi kuwa na wasiwasi kwamba biashara haingenoga wakati huu ambapo nchi na ulimwengu kwa jumla unakabiliana na ugonjwa wa Covid-19.

Kulingana na Bw Otieno, hatua yao ya kupeana nguo za bure ni mojawapo ya mbinu za kuonyesha shukrani kwa wateja hao.

“Tumefurahia sana. Licha ya uchumi kusambaratika kutokana na janga la corona, wateja wetu bado walijitahidi na kunogesha biashara zetu,” amesema Bw Otieno.

Naye muuzaji Bi Lucy Wairimu amesema kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na pia Eid al-Fitr mwaka huu kilikuwa tofauti ikilinganishwa na miaka iliyopita.

“Miaka iliyopita wateja waliozuru vibanda vyetu kununua bidhaa walikuwa wengi na pia walikuwa na pesa. Mwaka huu mambo ni tofauti. Wengi waliotembelea vibanda vyetu walikuwa kidogo na pia hawakuwa na fedha za kutosha. Tunatarajia hali itaimarika zaidi punde Covid-19 itakapodhibitiwa,” akasema Bi Wairimu.