Waislamu wamiminika madukani Lamu kununua nguo na bidhaa muhimu kwa maandalizi ya Idi
Na KALUME KAZUNGU
WAUMINI wa dini ya Kiislamu katika Kaunti ya Lamu wamemiminika madukani kununua nguo na bidhaa muhimu zikiwemo vyakula tayari kuadhimisha sherehe za Eid al-Fitr.
Sherehe hizo zinatarajiwa kuadhimishwa ama Jumamosi au Jumapili, lakini hili linategemea kuonekana kwa mwezi.
Wateja wengi wameshuhudiwa katika maduka ya nguo, sokoni na vibanda vingine vya kibiashara ili kujinunulia mapochopochio ya siku ya Idi.
Baadhi ya wale waliozungumza na Taifa Leo wamesema imewawia vigumu kupanga foleni ili kununua bidhaa wanazohitaji kwani hali hiyo inawapotezea wakati.
Mkazi wa Bajuri mjini Lamu Bi Salma Ahmed amesema yeye amekuwa akitangamana na wateja wenzake masokoni na kwamba hana wasiwasi wowote kwani yeye huvaa barakoa kila wakati awapo katika maeneo ya umma.
“Wakati huu wa matayarisho ya Idi, watu wamekuwa wengi na kwa kiasi inakuwa vigumu kusubiri, lakini maadamu tuna barakoa, sioni tatizo,” amesema Bi Ahmed.
Baadhi ya wamiliki wa maduka ya nguo wamesema wamekuwa wakizingatia sheria na kanuni zilizowekwa na Wizara ya Afya katika kuhudumia wateja wao.
“Tuko na maji na sabuni na japo wateja ni wengi, sisi huwahimiza wanawe mikono kwanza ndipo tuwahudumie japo kuna baadhi yao huwa wanaghairi kufanya hivyo,” amesema Bw Mohamed Suleiman.
Wakati huo huo, biashara mjini Lamu na viungani mwake zimekuwa zikifanya vyema juma hili la kumi la mwisho Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Bi Fatma Ali ambaye ni mmiliki wa duka la nguo kwenye mtaa wa Langoni kisiwani Lamu amesema wamerekodi faida kubwa kwani wateja wamekuwa wakizuru vibanda vyao na kununua nguo kwa wingi tayari kwa maandalizi ya Eid al-Fitr.
“Tunashukuru sana. Wateja ni wengi. Bidhaa zetu tumekuwa tukiuza kwa wingi hasa juma hili la kufunga mwezi wa Ramadhan. Tumepata faida kubwa,” amesema Bi Ali.
Kisiwa cha Lamu ni ngome kuu au kitovu cha waumini wa dini ya Kiislamu ikilinganishwa na maeneo mengine ya kaunti hiyo.