Habari

Wakazi wa Mokowe katika kaunti ya Lamu wakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji

January 22nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na KALUME KAZUNGU

ZAIDI ya wakazi 3,000 wa kijiji cha Mokowe na maeneo jirani, Kaunti ya Lamu wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji kufuatia kiangazi kinachoshuhudiwa eneo hilo siku za hivi karibuni.

Wakazi hao kwa miaka mingi wamekuwa wakitegemea maji kutoka kwa visima.

Aidha, kufuatia kiangazi kinachoshuhudiwa, zaidi ya visima 30 eneo hilo maji yake yamegeuka kuwa ya chumvi, hali ambayo imewaacha wakazi wakihangaika.

Katika mahojiano na wanahabari mjini Mokowe Jumanne, wakazi walisema wanalazimika kutembea masafa marefu wakitafuta maji, ambapo maji hayo yanapopatikana huwa yanauzwa kwa bei ghali.

Mkazi wa Mokowe, Bi Khadija Yusuf, anasema mara nyingi wamekuwa wakisafirisha maji kutoka eneo la Hindi huku wengine wakivukisha maji hayo wakitumia boti na mashua kutoka kisiwa cha Lamu hadi mjini Mokowe.

Bi Yusuf anaiomba serikali ya kaunti kuwasambazia maji kwa kutumia malori badala ya kuwaacha wakiteseka.

“Tangu maji ya visima vyetu yalipogeuka kuwa ya chumvi kufuatia kiangazi, hatuna tegemeo lingine ila kusafiri mbali na karibu kutafuta maji hayo. Maji yenyewe kuyapata na kuyasafirisha huwa ni ghali mno. Ombi letu kwa serikali ya kaunti ni kwamba badala ya kunyamaza, wafikirie jinsi tutakavyosambaziwa maji hapa Mokowe hata kama itamaanisha kupitia malori,” akasema Bi Yusuf.

Naye Bi Kahunda Charo alisema familia nyingi mjini Mokowe ni za kipato cha chini na kwamba haziwezi kukimu gharama ya kusafirisha maji kutoka sehemu za mbali.

Badala yake, familia hizo zimelazimika kutumia maji ya chumvi kutoka kwa visima, hatua ambayo tayari imechangia watoto na hata watu wazima kuugua maradhi ya ngozi na pia meno kubadilika rangi.

“Watoto wetu na sisi wenyewe hapa tunaugua maradhi ya ngozi na pia meno kubadilika rangi. Haya yote yanatokana na matumizi ya maji chafu. Tunahitaji suluhu ya haraka nay a kudumu ili tupate maji safi ya kunywa,” akasema Bi Charo.

Katika vijiji vya Bar’goni, Basuba, Milimani, Mararani, Mangai na Kiangwe, wakazi pia wamekuwa wakikabiliwa na tatizo hilo hilo la uhaba wa maji huku baadhi yao wakilazimika kuomba maji kwenye kambi za jeshi na polisi eneo hilo.

Baadhi ya wakazi pia wamelazimika kutumia maji ya Bahari Hindi ambayo ni ya chumvi kwa matumizi ya nyumbani.