Wakenya wanaamini machifu kuliko mawakili – Utafiti
Na BENSON MATHEKA
Kwa ufupi:
- Ni asilimia 7 pekee ya Wakenya 6005 walioshirikishwa wanaotafuta ushauri wa kisheria kutoka kwa mawakili
- Ingawa watu wengi wanaamini machifu kwa mizozo ya kifamilia, wengi wao huanza kwa kutafuta ushauri kutoka kwa watu wa familia zao
- Ni watu walio na elimu ya juu, matajiri au wanaochukuliwa kuwa matajiri wanaotafuta ushauri wa kisheria kutoka kwa mawakili
- Asilimia 25 hawakutafuta habari au ushauri wa kisheria katika kipindi cha miaka minne iliyopita licha ya kukabiliwa na matatizo
WAKENYA wengi wanawaamini machifu zaidi kuwapa habari za masuala ya kisheria kuliko mawakili na hata mahakama, utafiti unaonyesha.
Kwa jumla, asilimia 54 ya Wakenya hutumia asasi za serikali kupata habari kuhusu masuala ya kisheria huku wengi wao, ikiwa ni asilimia 19, wakiamini machifu.
Utafiti kuhusu mahitaji ya haki na uridhishaji wa mfumo wa haki unaonyesha kuwa ni asilimia 7 pekee ya Wakenya 6005 walioshirikishwa wanaotafuta ushauri wa kisheria kutoka kwa mawakili.
Asilimia 13 hutafuta ushauri kutoka kwa maafisa wa polisi na asilimia 8 kutoka mahakamani.
Kulingana na utafiti huo uliofanywa na shirika la Hague Insistute for Innovation of Justice (Hiil) kwa ushirikiano na Taasisi ya Mafunzo ya Mahakama ya Kenya (JTI), asilimia 41 ya Wakenya huwa wanatafuta ushauri kwa watu wa familia, marafiki na taasisi zizo za kisheria.
“Kwa kesi zinazohusiana na ardhi, watu hupenda kwenda kwa machifu au mahakamani. Kwa mizozo na majirani, watu huenda kwa chifu ambaye wanaamini atawasaidia. Pia chifu hutatua mizozo ya kifamilia,” unasema utafiti huo.
Maafisa wa Mahakama wanasema utasaidia kuimarisha utoaji haki nchini Kenya.
Marafiki
Kwa wanaokabiliwa na matatizo ya kikazi, utafiti huo unaeleza kuwa, huwa wanaamini marafiki na wafanyakazi wenzao kwa ushauri. Ingawa watu wengi huwa wanaamini machifu kwa mizozo ya kifamilia, utafiti ulifichua wengi wao huanza kwa kutafuta ushauri kutoka kwa watu wa familia zao.
Watafiti waligundua kwamba watu wengi nchini Kenya wanaamini polisi na machifu wanaoweza kuwasaidia katika kesi za uhalifu. “Kuhusu mizozo ya kifedha, watu wengi huwa wanatafuta habari na ushauri kutoka kwa marafiki,” unaeleza utafiti huo.
Miongoni mwa watu 6005 walioshirikishwa kwenye utafiti huo, asilimia 25 hawakutafuta habari au ushauri wa kisheria katika kipindi cha miaka minne iliyopita licha ya kukabiliwa na matatizo tofauti.
Baadhi yao walisema wanafikiri hata wakitafuta ushauri, hawangesaidiwa, wengine walisema hakuna ushauri ambao ungewasaidia au hawangemudu gharama ya kutafuta ushauri wa kisheria.
“Kwa masuala ya uhalifu, asilimia 45 walisema hawaamini hatua zozote zitachukuliwa wakipiga ripoti. Hii inaonyesha wazi kutamaushwa kwa watu hao na mfumo wa haki. Kwa mizozo ya ardhi, kizingiti sio kushindwa kumudu gharama ya huduma za kisheria,” unasema utafiti huo.
Uhamasisho
Unapendekeza uwekezaji zaidi kuhamasisha watu kuhusu masuala ya kisheria na upatikanaji wa habari na ushauri wa kisheria kutoka kwa wataalamu.
“Kizingiti kikubwa cha kutafuta habari na ushauri wa kisheria ni dhana kuwa hakuna hatua zitakazochukuliwa licha ya kupata ushauri au ukosefu wa usalama katika kutafuta ushauri huo,” unaeleza utafiti huo.
Unafichua kwamba ni watu walio na elimu ya juu, matajiri au wanaochukuliwa kuwa matajiri wanaotafuta ushauri wa kisheria kutoka kwa mawakili huku wale walio na elimu ya chini wakiwaendea machifu.
Kesi nyingi za kifamilia, unaeleza utafiti huo, huripotiwa miongoni mwa watu wa mapato ya chini. Asilimia 60 ya watu wasio na mapato ya kutosha walisema waliathiriwa na kesi hizo.
Aidha, ni watu walio na elimu ya kiwango cha chini wanaoathiriwa na kesi za unyakuzi wa ardhi ikiwa ni asilimia 30.