Wakenya wanavyopoteza mabilioni kwa wauzaji laghai wa mashamba
WAKENYA wengi wanaendelea kuishi katika umaskini baada ya kupoteza mabilioni ya pesa kwa walaghai wakinunua mashamba.
Haya yanajiri huku mahitaji ya kumiliki ardhi miongoni mwa wananchi yakizidi kuongezeka.
Kinaya ni kuwa, wanaofaa kuwalinda raia dhidi ya ulaghai huo ndio wahusika wakuu.
Kwa mfano, Bw Erastus Gicheha, 59, amelazimika kusaka usaidizi kutoka kwa serikali ili kupata haki baada ya kulaghaiwa.
Baada ya kuathiriwa na ghasia za uchaguzi mkuu 2007-2008, mfanyakazi huyo wa zamani wa benki, ambaye wakati huo alikuwa akiishi na kufanya kazi mjini Kisumu, aliamua kuhamia mjini Nakuru.
Aliungana na marafiki zake wanne ambao pia walikuwa wamepoteza mali kutokana na machafuko hayo.
Baada ya kuhamisha familia yake Nakuru, marafiki hao watano waliamua kuuza mali yao ya Kisumu ili kununua ardhi nyingine Nakuru.
Akiwa huko rafiki yake mmoja John Kamau aliwafahamisha kwamba mwenzake alikuwa amepata shamba la ekari tatu katika eneo la kifahari la Milimani.
Alidai mwenzake huyo kwa jina Jane Waithera, alitaka ekari moja tu ilhali mmiliki ardhi alitaka kuiuza yote.
Marafiki hao wakajadiliana na kukubaliana waungane na mwenzao kununua ardhi hiyo ili wagawane.
Bw Gicheh, ambaye alikuwa akitoa ushahidi katika mahakama mnamo Desemba 3, 2024 alidokeza kwamba yeye pamoja na marafiki zake hao walimwendea Peter Njuguna Gitau – ambaye wakati huo alikuwa mbunge wa Mwea – na kueleza nia yao ya kununua shamba hilo mnamo Machi 2008.
Baada ya kufanya upekuzi na uhakiki kutoka afisi ya ardhi pande hizo mbili zilifikiana kuhamisha umiliki wa ardhi hiyo katika iliyokuwa manispaa ya Nakuru – kipande cha ardhi Block 17/652 – kwa gharama ya Sh4.5 milioni.
Wakati wa kugawa mali walituma hati zao kwa afisi ya ardhi jijini Nairobi ambapo ombi hilo lilikataliwa baada ya kufahamishwa kwamba ardhi husika ni ya mtu tofauti.
Walipigwa na butwaa kujua kwamba ardhi hiyo ingali imesajiliwa kwa jina la mbunge huyo wa zamani Bw Gitau.
Imetafsiriwa na WINNIE ONYANDO