Habari

Wanafunzi 5700 waliopata C+ wakosa nafasi katika vyuo vikuu

April 10th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

WANAFUNZI 5,747 waliopata alama ya C+ kwenda juu kwenye Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili (KCSE) mwaka uliopita wamekosa nafasi ya kujiunga na vyuo vikuu vya umma, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa Jumatatu, Nairobi.

Waziri wa Elimu, Dkt Amina Mohamed, alitangaza kuwa ingawa jumla ya wanafunzi 69,151 walifuzu kujiunga na vyuo vikuu, kuna wanafunzi 2,128 kati yao ambao hawakujiandikisha kutengewa nafasi vyuoni ilhali wengine 3,619 walijiandikisha lakini wakakosa nafasi. Hivyo basi ni wanafunzi 62,851 waliopata nafasi.

Dkt Mohamed aliagiza shirika la kuchagua wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu nchini (KUCCPS) iwasiliane na wanafunzi hao mara moja na waruhusiwe kujiandikisha kujiunga na vyuo vikuu.

“Wizara imejitolea kuhakikisha hakuna mwanafunzi ambaye alifuzu atakosa nafasi katika vyuo vikuu vya umma. Naomba nipewe ripoti kuhusu wanafunzi hawa kabla wiki mbili zikamilike,” akasema, katika kongamano la wadau na uzinduzi wa mikakati maalumu ya KUCCPS.

Mbali na kuzingatia matokeo yao, wanafunzi walichaguliwa kwa msingi wa nafasi zilizopo katika vyuo vikuu vya umma nchini kwenye kozi mbalimbali na ukubwa wa miundomsingi ya vyuo.

Wanafunzi wengine 553 waliamua watafanya kozi za diploma licha ya kupata alama za kutosha kufanya digrii. Jumla ya wanafunzi 606,394 walifanya KCSE mwaka uliopita ambapo matokeo yalikuwa miongoni mwa mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa.

Kwenye mtihani huo, wavulana walipata matokeo bora kuliko wasichana na hivyo basi idadi ya wavulana watakaojiunga na vyuo vikuu ni 36,945 (asilimia 58.78) huku wasichana wakiwa 25,906 (asilimia 41.22).

 

Arafa

“Wale wote waliopata nafasi wataarifiwa kupitia kwa ujumbe mfupi wa simu au mtandao wa KUCCPS au wanaweza kuthibitisha kwenye mtandao wa KUCCPS,” akasema waziri.

Idadi ya wanafunzi watakaofanya kozi za Sayansi, Teknolojia na Hesabu (STEM) ni 28,135, huku watakaofanya kozi za kijamii ni 34,716.

Miongoni mwa watakaofanya kozi za STEM ni wavulana 19,156 (asilimia 31.91) na wasichana 8,979 (asilimia 68).

Dkt Mohamed alisema wanafunzi 971 kutoka maeneo yanayokumbwa na changamoto za kimaisha walichaguliwa kujiunga na vyuo vikuu bila kuzingatia alama zao pekee.

Wanafunzi 100,906 waliopata kati ya alama ya C na C- watasomea kozi za diploma na cheti cha kwanza cha elimu ya juu, huku wanafunzi 28,866 wakijiunga na vyuo vya kiufundi.

Waziri alihimiza wanafunzi waliopata alama za chini zaidi pia wajiandikishe kujiunga na vyuo vya kiufundi.

Wakati huo huo, alionya kuwa serikali haitasita kufunga vyuo vikuu ambavyo vimeshindwa kuboresha mandhari ya elimu ipasavyo.