Wandani wa Ruto wamiminika kwa Mudavadi
Na BENSON MATHEKA
IDADI ya wandani wa Naibu Rais William Ruto wanaomtembelea kiongozi wa Chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, ilizidi kuongezeka Alhamisi.
Matukio hayo katika makao makuu ya ANC jijini Nairobi, yameibua mjadala kuhusu uwezekano wa Bw Mudavadi kuungana na Dkt Ruto wakati ambapo siasa za Uchaguzi Mkuu wa 2022 zimeshika kasi.
Ingawa Bw Mudavadi amekanusha kuwa anapanga kushirikiana kisiasa na Dkt Ruto, kuendelea kukutana na washirika wa kisiasa wa Dkt Ruto kumeibua maswali hasa wakati huu ambapo Naibu Rais anaonekana kupigwa via ndani ya Jubilee.
Jana, makamu huyo wa zamani wa rais alikutana na mbunge wa Kimilili Didmus Barasa katika ofisi yake mtaani Lavington, Nairobi.Bw Baraza ni mmoja wa wandani wa Dkt Ruto eneo la Magharibi ambalo ni nyumbani kwa Bw Mudavadi.
“Tulijadili miongoni mwa masuala mengine mabadiliko ya kisiasa yanayoibuka nchini miongoni mwa mambo mengine kuhusu demokrasia, mikakati na maono ya kufufua uchumi unaodorora,” Bw Mudavadi alisema baada ya kukutana na mbunge huyo.
Wandani wengine wa Dkt Ruto kutoka eneo la Magharibi ambao amekutana nao ni John Walukhe wa Sirisia na Benjamin Washiali wa Mumias.
Wiki iliyopita, Bw Mudavadi alikutana na Gavana wa Uasin Gishu Jackson Mandago ambaye ni mwandani wa miaka mingi wa Dkt Ruto.
Kulingana na Bw Walukhe, mazungumzo yake na Bw Mudavadi yalihusu ambaye hujitaja kuwa sauti pekee ya upinzani, pia alikutana na Seneta wa Bungoma Moses Wetangula katika kile ambacho duru zinasema ni juhudi za kufufua mjadala umoja wa jamii ya Waluhya.