Habari

Watamsaliti Ruto?

May 22nd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

HARAKATI za kumng’oa Naibu Spika wa Seneti Kithure Kindiki leo Ijumaa ziliendelea kushika kasi jana Alhamisi maseneta sita wanaokabiliwa na hatari ya kufurushwa kutoka kwa chama cha Jubilee wakiripotiwa kuwa miongoni mwa maseneta 49 ambao wametia saini hoja ya kumwondoa.

Maseneta hao maalum ni miongoni mwa baadhi ya waliosusia kikao kilichoandaliwa na Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu juma lililopita.

Maseneta hao ambao wamekuwa wakiegemea upande wa Naibu Rais William Ruto pamoja na wale wanaotoka Mlima Kenya, anakotoka Profesa Kindiki, wameonekana kuchukua mkondo tofauti kufuatia presha kutoka Rais Uhuru Kenyatta.

Na Kiranja wa Wengi Seneta Irungu Kang’ata alikariri Alhamisi kuwa licha ya pingamizi kutoka kwa maseneta na wabunge wandani wa Naibu Rais William Ruto, hoja hiyo itajadiliwa leo Ijumaa na kuamuliwa kwani “ina uungwaji mkubwa.”

Maseneta hao maalum, Millicent Omanga, Falhada Iman, Naomi Waqo, Victor Prengei na Mary Seneta na Christine Zawadi hawakuhudhuria mkutano huo wa Ikulu ambao ulitekeleza mabadiliko katika uongozi wa Jubilee kwa kuwaondoa Kipchumba Murkomen na Susan Kihika kutoka nyadhifa za kiongozi wa wengi na kiranja wa wengi, mtawalia.

Kando na Bi Zawadi ambaye aliomba msamaha na kusamehewa, wengine watano wanatarajiwa kufika mbele ya kamati ya nidhamu ya Jubilee Jumatatu, Mei 25, 2020, kujitetea.

“Mkutano wa PG (kundi la wabunge na maseneta) sio mchezo. Maamuzi ya mkutano kama huo yametumiwa kuwaondoa viongozi mamlakani katika mataifa mengi duniani. Ukifeli kuhudhuria mkutano wa PG inaonyesha kuwa huna imani kwa uongozi wa chama,” Bw Kang’ata akasema kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge.

Maseneta wengine ambao wametia sahihi hoja hiyo ni pamoja na Njeru Ndwiga (Embu), Margaret Kamar (Uasin Gishu) na Mercy Chebeni (seneta maalum) ambaye pia anatoka kaunti ya hiyo anakotoka Dkt Ruto.

“Nimetia saini hoja hiyo kwa sababu huo ni msimamo wa chama chetu cha Jubilee. Hii ni licha ya kwamba Profesa Kindiki ndugu yangu kutoka eneo la Mlima Kenya,” Bw Ndwiga akasema.

Kiongozi wa wacheche James Orengo amewaongoza maseneta 14 wa ODM kutia saini hoja hiyo ambayo pia imepata uungwaji mkono kutoka kwa wenzao watatu kutoka Wiper na watatu kutoka Kanu.

Maseneta wa ANC George Khaniri (Vihiga) na Petronilla Were (maalum) pia wameweka sahihi yao katika hoja hiyo.

Kulingana na kipengele cha 106 (2) (c) cha Katiba, hoja kama hiyo inahitaji kuungwa mkono na thuluthi mbili ya idadi jumla ya maseneta 67 na ambayo ni maseneta 45. Hii ina maana kuwa hatima ya Profesa Kindiki tayari imeamuliwa kwa tayari maseneta 49 wametia saini hoja hiyo.