Watetezi raia, au wabinafsi?
Na BENSON MATHEKA
VITA vikali vya kisiasa kati ya Naibu Rais William Ruto na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga vinaongozwa na ubinafsi, wala sio maslahi ya wananchi, wadadisi wanaeleza.
Aliyekuwa Naibu Spika, Farah Maalim anasema wawili hao wanapigania maslahi yao wenyewe, na wale wanaodhani kuna vita kati ya wanasiasa hao au wanapigania maslahi ya umma wanajidanganya.
“Usidhani hawa wanapigania maslahi ya wananchi. wanajipigania wenyewe,” alisema Bw Maalim kwenye Twitter.
Malumbano ya Dkt Ruto na Bw Odinga yalianza kufuatia ‘handisheki’ mnamo Machi 9, 2018.
Mara baada ya mwafaka huo kati ya Bw Odinga na Rais Uhuru Kenyatta, Dkt Ruto na wanasiasa wa karibu naye walionya kuwa Bw Odinga alikuwa na nia ya kuingia serikalini kwa njia za mkato, na pia kuvunja chama cha Jubilee.
Japo nchi ilitulia baada ya ‘handisheki, wadadisi wanasema muafaka huo na malumbano yaliyofuatia kati ya Bw Odinga na Bw Ruto, yanaonyesha lengo kuu la wanasiasa hao ni kulinda maslahi yao ya kibinafsi, na hawana nia ya kutoa mazingira mwafaka ya maendeleo na vita dhidi ya ufisadi.
Kulingana na wadadisi, Bw Odinga na Dkt Ruto wana azma ya kugombea urais 2022 na hivyo kila mmoja anaelekeza juhudi zake kuona kwamba atamrithi Rais Kenyatta akikamilisha kipindi chake cha pili.
Dkt Ruto pia anataka kuthibiti siasa za eneo la Rift Valley.
Kwa kufanya hivi atahakikisha himaya yake ya kibiashara, ambayo amejenga itakuwa salama.
Kwa miaka mingi familia ya Rais Mstaafu Daniel Moi imekuwa ikitawala siasa za Rift Valley na Dkt Ruto anapigana kuhakikisha ameizima.
Mbunge mmoja wa Rift Valley alisema Naibu Rais anaamini Bw Odinga atatishia utajiri wake akiwa Rais: “Kinachozua joto tunaloona sio kutetea maslahi ya umma. Hii ni kuhusu maslahi ya kibinafsi na kibiashara. Kumbuka pia kwamba familia za Kenyatta na Odinga zinamiliki biashara kubwa ambazo zinahitaji kulindwa. Ni lazima wahakikishe kwamba serikali itakayoingia mamlakani italinda maslahi yao.”
Kwa upande wake, Bw Odinga anafanya juu chini kuwa rais wa kwanza kutoka eneo la Nyanza, na kuhakikisha kuwa familia yake itaendelea kudhibiti siasa za eneo hilo na pia kulinda himaya ya biashara ya familia yake.
Amegombea urais mara nne bila kufaulu, na kulingana na wandani wake, ‘handisheki’ ilifufua matumaini yake yaliyokuwa yamefifia baada ya kushindwa kwenye uchaguzi wa 2017.
“Uliona alivyowatema viongozi wengine katika upinzani? Hakuna ubinafsi unaoshinda huo,” alisema mbunge mmoja wa chama cha Wiper.
Hii ni baada ya Bw Odinga kufanya ‘handisheki’ na Rais Kenyatta bila kuwahusisha washirika wake katika muungano wa NASA, licha ya ushirikiano waliokuwa nao katika uchaguzi wa 2017.
Washirika hao ni Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetangula.