Watu tisa waliopewa siku 90 kumpata mwenyekiti na makamishna sita wa IEBC
MCHAKATO wa uteuzi wa mwenyekiti na makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) sasa umeanza baada ya kuapishwa kwa wanachama wa jopo la kuendesha kibarua hicho.
Watu hao ni pamoja na Linda Gakii, Profesa Adams Oloo, James Misati, Nicodemus Kipchirchir Bore, Balozi Koki Muli na Carolene Kituku.
Wengine ni; Andrew Kipkoech Tanui, Kasisi Dkt Nelson Makanda na Fatuma Saman.
Tisa hao waliapishwa mapema Jumatatu Januari 27, 2025 katika majengo ya Mahakama ya Juu, Nairobi katika hafla fupi iliyoshuhudiwa na Jaji Mkuu Martha Koome.
Bi Koome aliwashauri kuendesha majukumu yao kwa umakini, akisisitiza kuwa wanahitaji kuwateua makamishna wenye kiwango cha juu cha maadili.
Watu wa kuaminika
“Wale makamishna mtakaowateua sharti wawe watu waadilifu, watakaoendesha majukumu yao kwa njia huru, isiyo ya mapendeleo na inayozingatia kanuni zilizowekwa katika Katiba yetu,” akasema.
“Kando na kwamba IEBC ni mojawapo ya tume za kikatiba, ni tegemeo letu katika kuhakikisha chaguzi zinaendeshwa kwa njia bora zaidi. Kwa hivyo, wanachama wa tume hii wanapasa kuwa watu wenye maadili, utaalamu wa kiwango cha juu na watakaoaminika na wadau wote katika mfumo mzima wa uchaguzi,” Jaji Mkuu Koome akasisitiza.
Awali, Rais William Ruto aliwateua wanachama wa jopo kupitia tangazo kwenye toleo maalum la gazeti rasmi la Serikali.
Hatua hiyo ilijiri siku tatu baada ya Mahakama ya Kiambu kufutilia mbali kesi ambayo ilikuwa imekwamisha uteuzi wa jopo.
Kwenye uamuzi alioutoa Ijumaa wiki jana, Jaji Dorah Chepkwony alizima kesi iliyowasilishwa na Boniface Njogu, akipinga uwakilisha wa kikabili wa orodha ya watu waliopendekezwa kuwa wanachama wa jopo na kutojumuishwa kwa watu wanaoishi na ulemavu katika orodha hiyo.
Akiwateua wanachama hao tisa wa jopo hilo jipya, Rais Ruto pia alifutilia mbali tangazo la gazeti rasmi la serikali la Machi 2, 2023 ambalo kwalo wanachama saba wa jopo la zamani waliteuliwa.
Baada ya kuapishwa kwa wanachama wa jopo jipya la kuteua makamishna wa IEBC Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula aliamwagiza Katibu wa Tume ya Huduma za Bunge (PSC) Jeremiah Nyegenye kuweka tayari mahitaji yote yatakayoliwezesha jopo hilo kutekeleza majukumu yake.
Gharama ya shughuli za jopo
“Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iliyofanyiwa marekebisho inahitaji tume ya PSC kutoa huduma za sekritariati na vifaa kwa Jopo hilo na pia kugharamia shughuli zake,” Bw Wetang’ula akaeleza, kwenye ujumbe kupitia mtandao wa kijamii wa X.
“Hili ni suala lenye umuhimu wa kitaifa na nitatoa wito kwa Jopo la Uteuzi kukamilisha mchakato wa uteuzi wa makamishna wapya wa IEBC haraka iwezekanavyo na kulingana na sheria,” Bw Wetang’ula akaongeza.
Kulingana sheria, jopo hilo lina muda wa siku 90 kukamilisha zoezi la uteuzi wa Mwenyekiti mpya na makamishna sita wa IEBC watakaoendeshwa uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika Agosti 9, 2027.
Rais Ruto aliwateua wanachama wa jopo hilio siku moja baada ya kuwekewa presha na viongozi wa upinzani wakiongozwa na Kalonzo Musyoka, wakisema kujivuta kwake kunaweza kulitumbukiza taifa hili katika mzozo wa kikatiba.
“Ikiwa kufikia Jumatatu (Januari 27, 2025) Ruto hatakuwa ameteua wanachama wa jopo la kuteua makamishana wa IEBC tutatoa taarifa kamili kuhusu suala hilo. Kesi imeondolewa na sasa hana sababu ya kutoteua wanachama wa jopo hili ili lianze kuteua makamishna wapya wa tume hii,” Bw Kalonzo akasema, Jumapili baada ya kuhudhuria ibada ya Jumapili katika kanisa moja eneo bunge la Dagoretti Kaskazini.
Waliompa Ruto ‘makataa’
Wengine waliotoa makataa kwa Rais Ruto kuhusu suala hilo ni Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni, Kiongozi wa chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) Eugene Wamalwa na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna.
Mchakato wa uteuzi wa makamishna wa IEBC ulikwama mnamo Julai 2023, baada ya serikali kuagiza jopo la zamani lililoongozwa na Dkt Makanda kusitisha shughuli hiyo ili kutoa nafasi kwa Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (Nadco) kutoa mwelekeo kuhusu suala hilo.
Hii ni baada ya mrengo wa Azimio uliongozwa na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga kudai Rais Ruto aliteua jopo hilo, kivyake, bila kufanya mashauriano na wadau wengine.