Habari

Wazazi waonywa dhidi ya kupeleka watahiniwa kwa wachawi

October 24th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na SHABAN MAKOKHA

MAAFISA wa elimu katika kaunti ndogo ya Mumias wameonya wazazi dhidi ya kuwahusisha wanafunzi wao katika ushirikina ili kupita mitihani yao ya Darasa la Nane (KCPE) na kidato cha nne (KCSE).

Afisa wa Elimu kaunti ndogo ya Mumias Magharibi, Bw Thomas Mukabi, na mwalimu mkuu wa shule ya upili ya wavulana ya Mumias Muslim, Bw Osman Osieko, walisema watahiniwa hawafai kusumbuliwa wakati huu wanapojitayarisha kwa mitihani.

“Tuache watahiniwa watumie masomo ambayo wamefunzwa darasani kufanya mitihani yao. Mbinu zingine zisizofaa zisitumike kamwe,” alisema Bw Osieko.

Vile vile, Bw Osieko alitahadharisha wazazi dhidi ya kuhadaiwa na matapeli wanaodai kuwauzia karatasi za mtihani.

Mumias Magharibi iko na jumla ya watahiniwa 3,406 watakaofanya mtihani wa KCPE wiki ijayo, na 2,410 wa KCSE ambao tayari walianza mtihani Jumatatu.

Bw Mukabi alisema maafisa wake wamejitayarisha vilivyo kwa mitihani hiyo ya kitaifa.

“Tumewapa maelezo yote wasimamizi wa vituo vya mitihani na wakuu wa mitihani na pia kutuma maafisa wa usalama kwa vituo hivyo; tuko tayari kwa mitihani ya kitaifa,” alieleza na kuonya wazazi na wanafunzi dhidi ya kujiingiza katika vitendo vitakavyohujumu matokeo yao.

Wazazi kadha wamejitokeza kudai kuwa uchawi umetumika katika baadhi ya shule wakati wa mitihani. “Shule kadha zimekuwa zikidorora katika mitihani kwa sababu ya wazazi kuhusisha wanafunzi wao katika uchawi,” akasema mzazi mmoja, Ezekiel Kuria.

Bw Kuria alisema wazazi hao huwapeleka wanafunzi kwa waganga wanapokaribia kufanya mitihani ya kitaifa wakilenga kuimarisha uwezo wao wa kufanya vyema.

“Ushirikina ungali umeteka wazazi wengine hususan wakati watoto wao wanapojitayarisha kwa mtihani wa kitaifa. Wanakimbilia uchawi ili kuwalinda watoto wao dhidi ya wapinzani na kutumai watafanya vyema kimasomo,” alieleza.

Bw Mukabi, alionya wazazi dhidi ya kukimbilia njia kama hizo za mkato akisema kamwe hazisaidii kuimarisha matokeo ya mtihani ya wanafunzi wala masomo yao kwa jumla.

Afisa huyo wa Elimu Mumias Magharibi alikemea vitendo hivyo akisema waganga na wachawi wamewateka wazazi kuwa wateja wa mara kwa mara ili kujinufaisha kiuchumi.

Aliongeza kuwa vitendo vya ushirikina vimesababisha wanafunzi kuduwaa darasani na kudorora kiafya.