Habari

Wito serikali iingilie kati kuwaokoa mwanaharakati Bob Njagi na mwenzake

Na SAMMY KIMATU October 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KUNDI la wanaharakati la Young Aspirants Movement (YAM), limekosoa vikali serikali ya Uganda kufuatia tuhuma za utekaji nyara wa wanaharakati wawili wa Kenya.

Kundi hilo limerejelea kitendo hih kama cha ‘aibu’ na cha kukiuka haki za binadamu.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Nairobi, Mwenyekiti wa Kitaifa wa YAM, Osteen Peter Ngui, alikosoa tukio hilo, akisema kwamba vitendo kama hivyo hudhoofisha Umoja na heshima kati ya nchi za Afrika Mashariki. Alisema kuwa utekaji nyara huo si tu ukiukaji wa uhuru wa binaadamu bali pia ni onyesho la kuporomoka kwa viwango vya haki za binadamu kote barani Afrika.

“Ni haki ya kila mtu kusafiri huru kwenda nchi yoyote, mradi tu atimize vigezo vya kisheria na vya uhamiaji,” alisema Ngui. “Kilichotokea si tu ukiukaji wa haki za wawili hao, bali ni doa kwa uongozi wa Afrika Mashariki. Kama kanda, tunakuwa mfano mbaya kwa bara la Afrika na dunia kwa ujumla.”

Ngui alisisitiza kuwa mataifa ya Afrika Mashariki yanapaswa kuimarisha maadili ya kidemokrasia na kinga za haki za binadamu badala ya kujihusisha na vitendo vinavyotishia au kuhatarisha sauti za raia.

Aliitaka serikali husika kushughulikia suala hilo kwa uwazi na kuhakikisha uwajibikaji.