Yabainika ujenzi wa jengo lilioua wanafunzi 7 ulikuwa duni
NA PETER MBURU
SHULE ya msingi ya Precious Talent Academy ambapo wanafunzi saba walifariki Jumatatu asubuhi baada ya sehemu ya jengo kubomoka ilikuwa katika hali mbaya, na kutokea kwa mkasa huo si muujiza, Taifa Leo Dijitali imebaini.
Majengo ya shule hiyo iliyoko wadi ya Ng’ando, Nairobi yako katika hali duni – mengi yakiwa ya mabati, licha ya kuwa zaidi ya wanafunzi 800 hufika humo kila siku kukata kiu ya elimu.
Shule yenyewe haina hata ua, na hivyo mtu yeyote anaweza kuingia kupitia popote.
Mwonekano wa sehemu ya jengo lililobomoka Jumatatu ulionyesha wazi kuwa lilikuwa dhaifu, kwani lilishikiliwa na miti miwili na chuma zilizokunjika pekee.
Baadhi ya wazazi na majirani wa shule hiyo walisema kuwa tayari walikuwa wameeleza hofu yao kuhusu usalama wa wanao, kutokana na hali mbaya ya majengo shuleni humo.
Wengi wamedai kuwa ujenzi mbaya ndio ulisababisha hali ya majengo shuleni humo kuwa dhaifu.
Brian Ajega, mkazi wa Ng’ando ambaye alijitokeza kusaidia katika uokoaji alisema kuwa ijapokuwa darasa la chini katika sehemu iliyobomoka lilikuwa limejengwa kwa mbao, madarasa yaliyokuwa juu yalikuwa yamejengwa kwa mawe.
Bw Meshack Nyabuto, mfanyakazi katika afisi ya chifu wa eneo hilo naye alisema kuwa baadhi ya wanafunzi walikuwa wamelalamika kuhusu hali ya jengo lenyewe kuwa likitikisika mara kwa mara, japo hakuna aliyewapa sikio.
Walipofika shuleni humo Jumatatu, maafisa kutoka Halmashauri ya Ukaguzi wa Majengo (NBI) walisema majengo hayo yalikuwa na makosa mengi, kwani utaratibu haukufuatwa wakati wa ujenzi.
Katibu wa NBI Moses Nyakiogora alisema maafisa wa halmashauri hiyo hawakuwa na habari kuhusu hali ya shule hiyo, akikiri kuwa kuna majengo mengi ya aina hiyo Nairobi.
Shirika la uokoaji la St John’s Ambulance lilisema “jingo hilo lilikuwa na madarasa manne chini na manne juu. Yalikuwa yamejengwa kwa mbao na mabati,” kupitia ujumbe kwa vyombo vya habari.
Lakini mmiliki wa shule hiyo Moses Wainaina alilaumu serikali ya Kaunti ya Nairobi kwa ajali hiyo, akisema ndiyo ilichimba mtaro wa kupitisha maji taka nyuma ya madarasa, hali iliyofifisha uthabiti wa jengo lenyewe.
Wengi wa walioangamia katika mkasa huo walikuwa wanafunzi wa madarasa ya kwanza hadi tatu, ambao walikuwa wakisomea katika madarasa ya juu.