Habari

Yaibuka Ruto ‘alimsindikiza’ Uhuru uchaguzini

January 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANDISHI WETU

HUENDA Rais Uhuru Kenyatta alisaidiwa na wataalamu wa kampuni iliyosimamia kampeni zake ya Cambridge Analytica, kumwekea mtego Naibu Wake William Ruto alipounganisha chama chake cha URP na TNA kubuni Jubilee Party kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Stakabadhi za siri zinaonyesha kuwa kampuni hiyo ilimshauri Rais Kenyatta jinsi ya kuendesha kampeni zake kupitia chama kimoja chenye nguvu ili zifanikiwe zaidi.

Katika kile kinachoonyesha kwamba Dkt Ruto alikuwa msindikizaji tu kwenye mipango ya kampeni, mikakati yote ya kampeni ilifanywa na kampuni hiyo na wandani wa Rais Kenyatta.

Waliopigia debe chama hicho kilipobuniwa, akiwemo Rais Kenyatta walidai kingeunganisha Wakenya na kumsaidia Dkt Ruto kumrithi 2022.

Dkt Ruto alishawishika licha ya baadhi ya wandani wake kutochangamkia hatua hiyo na kumshauri asivunje chama chake cha URP.

Kulingana na stakabadhi hizo, ni mshauri wa masuala ya kisiasa wa Rais Kenyatta Nancy Gitau na msaidizi binafsi wa Rais Kenyatta Jomo Gecaga ambao walikuwa wakishirikiana na kampuni ya Cambridge Analytica kuandaa kampeni ikiwemo kuunganishwa kwa vyama vya TNA na URP.

Wandani wa Dkt Ruto wamekuwa wakitaja Bi Gitau miongoni mwa maafisa wa serikali wanaohujumu azma yake na inasemekana alilazimika kujiuzulu kutoka afisi ya rais kufuatia presha kutoka kwa kambi ya naibu rais.

Mawasiliano kati ya kampuni hiyo na wandani wa Kenyatta yanamsawiri Bi Gitau kama aliyesimamia kampeni za Rais Kenyatta akishirikiana na Sabhita Raju wa Cambridge Analytica.

Bi Gitau alisaidiana na Bw Gecaga kupanga mikakati ya kampeni za Jubilee ambayo iliwekwa kwa siri kwa Wakenya wengine na hata wateja wa kampuni hiyo.

Wakati mmoja, afisa wa kampuni hiyo Brittany Kaiser alionya maafisa wenzake dhidi ya kuanika shughuli zao Kenya ili wasikasirishe wanamikakati wa Rais Kenyatta.

“Mnapaswa kukumbuka kuwa hatuwezi kutaja kazi yetu Kenya kwa Wakenya wengine. Ikifikia kundi la Kenyatta kwamba tunawaarifu wengine kuhusu kazi yetu, inaweza kuhatarisha moja ya kandarasi zetu kubwa,” inasema barua ya Kaiser.

Wadadisi wanasema matukio katika chama cha Jubilee baada ya uchaguzi mkuu wa 2017 ambapo Dkt Ruto anaonekana kutengwa serikalini, yanaonyesha huenda hakufahamu kilichomsubiri.

Wandani wa Rais Kenyatta walianza kuapa kumzuia kuwa Rais wakisema hakuna deni la kisiasa analopaswa kulipwa na wafuasi wa kiongozi wa nchi kwa kumsaidia kushinda uchaguzi mara mbili.

Rais Kenyatta ambaye wakati wa kampeni aliahidI kumuunga mkono Dkt Ruto kwenye uchaguzi wa 2022 amenukuliwa akisema ni Mungu anayejua atakayekuwa Rais wa nchi baada yake huku chama cha Jubilee kikikumbwa na mgawanyiko.

Stakabadhi zilizoanika mawasiliano kati ya wandani wa Rais Kenyatta na chama chake cha TNA, zinaonyesha kwamba mikakati ilitokana na tafiti zilizofanywa na kampuni hiyo na kufadhiliwa na Rais Kenyatta.

Katika nyaraka zake kuhusu uchaguzi mkuu wa Kenya 2013 na 2017, kampuni hiyo inaweka wazi kuwa ilikuwa ikifanyia kazi TNA na Rais Kenyatta ilichangia pakubwa kuunganishwa kwa TNA na URP.

“Kushinda uchaguzi enzi hizi, kunahitaji vyama vya kisiasa vinavyoweza kuendesha kampeni kubwa zilizoshirikishwa vyema kote nchini. Shughuli zinapaswa kupanuliwa hadi viwango vya juu chamani hadi kwa washirikishi wa kujitolea mashinani,” kampuni hiyo ilisema kwenye stakabadhi kwa Rais Kenyatta 2016.

Kampuni hiyo iliporomoka baada ya kufichuliwa kwamba iliendesha kampeni chafu kwenye uchaguzi mkuu Kenya 2013 na 2017 na mataifa mengine ulimwenguni.

Wadadisi wanasema masaibu anayopitia Dkt Ruto huenda yalipangwa wakati wa kuweka mikakati ya kampeni.