Dondoo

Hata umpe dhahabu, hupati mapenzi ya dhati

Na BENSON MATHEKA August 30th, 2024 2 min read

MACHALI wanatumia pesa au hadhi zao kwa vipusa ili wameze  chambo.

Unapata chali anatumia maelfu ya pesa na zawadi ghali kwa mwanadada ili aweze kumpenda.

Unachosahau kaka ni kuwa mapenzi hayawezi kununuliwa. Hayawezi hata kwa dhahabu.

Kile ambacho pesa zinafanya ni kutoa mazingira ya kufurahia mapenzi. Haziwezi kuyanunua.

Raha unayoponda na mwanadada anayekuchangamkia  unapomwangushia manoti sio mapenzi.

Ni anasa na inanyauka kama ua pesa zikiisha kisha uliyedhani anakupenda anaingia mitini na kuanguka kifuani cha alizonazo.

Mapenzi huwa yanastahimili hali zote. Kigezo cha kwanza ambacho demu mwenye mapenzi ya dhati anazingatia sio pesa za mwanaume, kwa kuwa hajiuzi.

Demu akikukataa na baada ya kumpa pesa au zawadi ya nguvu akuchangamkie na kukubali, kaka, umenunua mpenzi, sio kwamba anakupenda. Utajua ukweli, pesa zikiisha, au akirushiwa mistari na mwanaume mwingine aliye na pesa nyingi kukuliko.

Kosa jingine ambalo wanaume wanafanya ni kutumia ushawishi wa hadhi yao kuvutia vidosho. Demu akikukataa ukiwa mtu wa kawaida kisha akukubali hadhi yako ikipanda, sio wewe anapenda, ni hadhi yako na ukiivua au uivuliwe, hautamuona.

Hivyo basi, ikiwa hautaki kujuta, usitumie hadhi, cheo, au mamlaka yako kama chambo kwa mademu. Kwa hakika, ukitaka kurushia demu ndoano, usianike cheo chako hadi baada yake kukupa uamuzi wake.

Uamuzi huo ukiwa hasi na aubadilishe akijua cheo chako, muambae kama ukoma.

Kaka, ikiwa una mamlaka, usiyatumie kutisha demu ili akupende.

Hili ndilo kosa kubwa zaidi ambalo mwanamume anaweza kujifanyia na ambalo hufanyika.

Furaha ya uhusiano wa mapenzi ni wawili wanapopendana kutoka kwa moyo, sio kwa sababu ya vitisho.

Mwanamume wa kisawa sawa hutumia mistari kuingiza boksi mademu, sio vitisho.

Hili nalo ndilo kosa babu kubwa; kuamini kuwa demu atakuwa wako kwa sababu ya hisani unayomfanyia.

Kaka, mradi demu yuko kwa wazazi wake na hajafanya uamuzi wake binafsi kuwa wako, hata ukimfufua kutoka wafu, sio lazima awe mpenzi wako.

Kwa hivyo, utafanya kosa kubwa sana kuamini kwamba ukilipia demu karo ya shule au kumtafutia kazi atakukubali kuwa mpenzi wako moja kwa moja.

Demu akiwa kwa shida na uwe na uwezo wa kumsaidia na ufanye hivyo ukitarajia atakuwa mkeo, unaalika balaa.

Demu anafaa kukubali kwa sababu anakupenda, kwa sababu anakuchagua. Usitumie hisani kumlazimisha demu akupende.