Habari Mseto

Hatuungani kisiasa, lengo ni kukabili muguka – Omar

June 7th, 2024 2 min read

NA WINNIE ATIENO

NAIBU Mwenyekiti wa Chama cha UDA, Bw Hassan Omar, amefafanua kuwa, ushirikiano baina ya wanasiasa wa Pwani ambao ulionekana hivi majuzi ni wa kupambana na muguka pekee.

Bw Omar alipuuzilia mbali dhana kuwa huenda kukawa na muungano wa kisiasa wa viongozi wa Pwani hivi sasa, baada yao kuonekana pamoja hivi majuzi wakitoa kauli moja kuhusu hitaji la kupambana na uraibu wa muguka na miraa katika ukanda huo.

Kulingana na Bw Omar, viongozi wa Pwani wameamua kumuunga mkono Gavana Abdulswamad Nassir kuendeleza vita dhidi ya uraibu huo.

“Ushirikiano wetu si wa kisiasa bali ni wa vita dhidi ya muguka. Ikifika kwenye siasa, tunajua tutachukua uongozi bila hata kampeni,” alisema Bw Omar, akiwa eneobunge la Mvita kwenye kampeni za uchaguzi wa viongozi wa mashinani wa UDA.

Bw Nassir alianzisha mapambano dhidi ya uraibu wa muguka na miraa alipopandisha ada za kusafirisha bidhaa hizo Mombasa, kisha baadaye akapiga marufuku muguka, hatua iliyositishwa kwa muda na mahakama.

Baadaye, magavana Gideon Mung’aro (Kilifi) na Andrew Mwadime (Taita Taveta) pia walitangaza marufuku, huku Bi Fatuma Achani (Kilifi), ambaye ni mwanachama wa UDA, akitangaza ada za juu kwa biashara hizo ili kudhibiti uraibu.

Viongozi wengine wa UDA Pwani ambao waliunga mkono hatua hizo ni Naibu Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Taifa, Bw Owen Baya, na Waziri wa Jinsia, Bi Aisha Jumwa.

Bw Omar, ambaye pia ni Mbunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), alisisitiza kuwa azma yake ya kuwania ugavana 2027 dhidi ya Bw Nassir ingali imara hata kama wataonekana kuwa na msimamo mmoja kwa masuala mengine kwa sasa.

“Tunamwambia tu yeye ni ndugu yetu, tumekuwa naye, tumelelewa pamoja lakini sasa ilipofika, pale Kenya inapokwenda, na yale ambayo tunayoangazia huku mbele ya safari yeye sasa atulie,” alisema Bw Omar.

Seneta huyo wa zamani wa Mombasa ambaye amepigania ugavana kaunti hiyo mara tatu bila mafanikio, alidai kuwa safari hii itakuwa ‘mswaki’ kwake kwani kinara wa ODM, Raila Odinga, na aliyekuwa gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho, wana majukumu mengine makubwa kuliko kufuatilia siasa za Pwani.