HabariHabari za Kitaifa

Hofu mitihani itavurugwa walimu wakishikilia watagoma

Na VITALIS KIMUTAI August 11th, 2024 2 min read

WALIMU nchini wameshikilia kuwa hawatalegeza msimamo wao na kwamba wataendelea na mgomo wao shule zikifunguliwa hadi Mkataba wa Makubaliano ya Pamoja wa 2021-2025 (CBA) uliotiwa saini na Tume ya Huduma ya Walimu (TSC) utakapotekelezwa.

Hii ni baada ya bunge kukosa kuongeza Sh13.3 bilioni katika bajeti ya ziada iliyoidhinishwa na Rais William Ruto wiki jana kwa utekelezaji wa awamu ya pili ya makubaliano hayo.

Awamu ya pili ya makubaliano hayo iliyotiwa saini mwaka 2021 na mwaka 2023 ilianza kutumika Julai 1, 2024, huku awamu ya kwanza – inayohusu mishahara na marupurupu ya walimu – ikiwa tayari imeshatekelezwa.

Bw Collins Oyuu, Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT) na Makamu Mwenyekiti wa Kwanza wa Kitaifa Malel Langat walisikitika kwamba wakisema walimu watalazimika kukosa kufungua shule muhula wa tatu hadi makubaliano hayo yatimizwe.

Bw Oyuu na Bw Langat walisema inasikitisha kwamba bunge limeshindwa kusikiliza maombi ya walimu ili kuepusha mzozo katika sekta ya elimu.

“Tulizungumzia suala hilo kwa Kamati ya Bajeti na Matumizi chini ya uenyekiti wa Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro na mwenzake Julius Melly (Mbunge wa Tinderet) ili kuhakikisha mgao wa fedha kwa walimu hauchezewi kwani hiyo italeta fujo kwa walimu. Lakini inaonekana hawakusikiliza,” Bw Oyuu alisema.

“Hatutarudi nyuma katika jitihada za kuhakikisha utekelezaji kamili wa CBA kwani ni haki yetu. Hakuna jinsi makubaliano ya kisheria katika Mahakama ya Ajira na Mahusiano ya Kazi yanaweza kujadiliwa upya,” Bw Oyuu alisema.

Bw Langat alisema TSC itadharau mahakama ikiwa itakosa kutekeleza CBA kwa walimu kwani hati hiyo ni halali na imetiwa saini na Katibu Mkuu wa KNUT, mwenyekiti wa kitaifa, Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume na mwenyekiti.

‘Katika ugawaji wa fedha hizo, jambo la kwanza kuzingatiwa lilipaswa kuwa pesa za utekelezaji wa CBA ambayo hutoa nyongeza ya mishahara kwa walimu humu nchini,’ Bw Langat alisema.

“Hakuwezi kuwa na maendeleo yoyote ya maana katika nchi yoyote bila kuzingatia sekta ya elimu,” Bw Oyuu alisema.

Tishio la walimu hao kutumia mgomo ili kuishinikiza serikali kutekeleza madai hayo, linasababisha hali ya suitafahamu huku nchi ikikumbwa na maandamano ya vijana dhidi ya serikali wakipinga sera nyingi za kiuchumi.