Habari za Kitaifa

Hurumia kijana yetu Kindiki, wazee waambia Ruto wakimsihi amteue tena serikalini

Na GITONGA MARETE July 15th, 2024 2 min read

VIONGOZI kutoka kaunti za Tharaka Nithi na Meru wamemwomba Rais William Ruto kumpa aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Profesa Kithure Kindiki nafasi tena atakapoteua baraza jipya la mawaziri.

Gavana wa Tharaka-Nithi Muthomi Njuki,  Spika wa bunge la kaunti hiyo John Mbaabu na mwenzake wa Meru Ayubu Bundi Jumapili walisema Profesa Kithure alikuwa akiongoza katika kuchapa kazi kwenye baraza la mawaziri lililovunjwa na Rais wiki jana kwa hivyo anastahili kuteuliwa tena.

Wanasiasa hao walisema kuwa hakuna kiongozi yeyote mwenye hadhi ambaye amehitimu kutoka Mlima Kenya Mashariki anaweza kuhudumu kama waziri kando na Profesa Kindiki.

Bw Njuki alisema Profesa Kindiki alipambana sana kuhakikisha kuna usalama nchini ikiwemo kuwatimua magaidi na pia majangili ambao walikuwa wamesababisha ukosefu wa usalama ukanda wa Kaskazini mwa Bonde kwa miaka na mikaka.

“Wakenya wanaunga hatua aliyoichukua Rais ya kuvunja baraza la mawaziri na kauli yake kuwa atashauriana na washikadau wote kabla ya kuteua baraza jipya,” akasema Bw Njuki.

Alikuwa akiongea wakati wa ibada ya shukrani katika kanisa la PCEA Jennifer Njuki kwenye eneobunge la Chuka/Igambang’ombe.

“Wadhifa wa uwaziri aliokuwa akiushikilia ulitengewa Mlima Kenya na tumeketi na kukubaliana kuwa arejeshewe wadhifa huo. Tunaamini kuwa Rais atatusikia,” akaongeza.

Gavana huyo aliteta na kusema kuwa Profesa Kindiki hakupatikana na hatia yoyote ya kutumia afisi vibaya au kosa jingine akiwa waziri wa usalama wa ndani.

Alilia kuwa Kinara wa Upinzani Raila Odinga huenda akasababisha Rais kumtimua Profesa Kindiki ilhali ni aliyekuwa Inspekta Jenerali wa polisi Japhet Koome ndiye anastahili kufutwa kabisa kwa kuwatumia polisi vibaya wakati wa maandamano.

“Koome amekubali kuchukua majukumu kutokana na maovu ya polisi dhidi ya waandamanaji. Rais asikubali msimamo wa Raila Odinga kuwa Profesa Kindiki pia afutwe kutokana na mauaji yaliyotekelezwa na polisi,” akasema.

Bw Mbaabu aliunga kauli ya Bw Njuki wa kusema Profesa Kindiki anastahili kurejeshewa wadhifa wake. Alisema kuwa waziri huyo na Bw Njuki ndio sauti ya kisiasa ya wakazi wa Tharaka-Nithi.

Kwa upande wake Bw Bundi alisema uongozi wa kaunti za Meru na Tharaka-Nithi utaendelea kushinikiza Profesa Kindiki arejeshewe wadhifa wake katika baraza jipya la mawaziri.

Viongozi hao walikubali kuwa upepo wa Gen Z ni mkali na ulichangia kutimuliwa kwa Profesa Kindiki na wenzake japo wakakiri masuala yanayoibuliwa na vijana ni mazito na yanastahili kutatuliwa.