Habari Mseto

Idadi ya waliofariki katika ajali Kisumu yapanda hadi 17

January 29th, 2024 1 min read

OUKO OKUSAH Na ELIZABETH OJINA

WATU 17 wameaga dunia kufuatia ajali iliyotokea saa nane na nusu usiku mkuu kuamkia Jumatatu katika eneo la Othoo, Nyando katika Kaunti ya Kisumu.

Ajali ilihusisha lori na basi la Super Metro, ambalo walioshuhudia ajali hiyo walisema lilikuwa likielekea Mombasa.

Ajali ilitokea basi lilipokuwa linapita motokaa ndogo na ghafla likagongana na lori la mpunga.

Madereva wa magari yote mawili waliaga dunia papo hapo.

“Tuliamsha na sauti ya kishindo na tulipowahi eneo la ajali tumekutana na mabaki ya basi na lori yakiwa yemetapakaa barabarani. Abiria waliokuwa na majeraha walikuwa wakilia kwa maumivu ya majeraha waliopata,” akasema Bw James Onyango, mkazi wa eneo hilo.

Mkazi mwingine, Bw Peter Otieno alisema walifanikiwa kuona miili 11 ukiwemo wa mvulana wa umri wa miaka mitano.

“Tulisumbuka sana kuondoa mwili wa dereva wa lori kwa sababu lilikuwa limeharibika vibaya,” akasema Bw Otieno.

Polisi kutoka kituo cha polisi cha Ahero walifika katika eneo la ajali wakasaidiana na wasamaria wema kuondoa miili na kunusuru waliopata majeraha.

Soma Pia: Watu 11 wapoteza maisha katika ajali Ahero

Kwa mujibu wa naibu msimamizi wa idara ya afya katika Kaunti ya Kisumu Ibrahim Wanyande, abiria 12 waliopata majeraha madogo walitibiwa na kuruhusiwa kuondoka.

“Watu 15 wanaendelea kutibiwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga. Wawili wako katika hali mahututi,” akasena Bw Wanyande.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Ahero Grace Thuo aliambia Taifa Leo kwamba miili 12 ilipelekwa katika mochari ya hospitali ya Ahero.

Bi Thuo alisema wangali wanafuatilia kujua idadi kamili ya abiria waliokuwa katika basi hilo wakati ajali hiyo ilitokea.