Habari za Kitaifa

IG Kanja: Nitatia adabu polisi mafisadi  

Na NDOBI MUTORI August 16th, 2024 1 min read

INSPEKTA Jenerali wa Polisi (IG) Mteule Douglas Kanja ameahidi kutekeleza mageuzi makubwa katika Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) iwapo uteuzi wake utaidhinishwa na Bunge.

Kwanza, Bw Kanja, 60, Alhamisi, Agosti 15, 2024 aliwaahidi wabunge na maseneta waliokuwa wakimhoji kubaini ufaafu wake kwa wajibu huo, kwamba atapambana vikali na zimwi la ufisadi kwenye polisi.

Alisema atafanya hivyo kwa kuimarisha uwazi na uwajibikaji katika udumishaji usalama kwa kuamuru maafisa wote wavalie beji zenye majina yao wakiwa kazini.

“Aidha, nitapambana na polisi wanaoshirika mgongano wa kimasilahi wakiwa kazini. Polisi watalazimika kuamua kufuata mkondo mmoja,” akasema Bw Kanja ambaye amehitimu kwa shahada ya digrii katika Biashara.

“Nilipohudumu kama Naibu Inspekta Jenerali, niligundua kuwa baadhi ya maafisa wa polisi ndio wamiliki wa matatu zinazovunja sheria au mabaa yanauza pombe haramu. Niliwaambia kufuata mkondo mmoja, kuacha kazi ya polisi na kuendesha biashara ya matatu au kuacha biashara ya matatu na kujishughulisha na kazi katika NPS,” Bw Kanja, ambaye amehudumu kama afisa wa polisi kwa miaka 39, akaambia Kamati ya Pamoja ya Bunge la Kitaifa na Seneti iliyokuwa ikimpiga msasa Alhamisi katika majengo ya bunge.

Endapo, kamati hiyo na mabunge yote mawili yataidhinisha uteuzi wake, Bw Kanja atachukua nafasi ya Japhet Koome aliyejiuzulu Julai 12, 2024.

Imetafsiriwa na Charles Wasonga