Habari Mseto

IMF yakasirishwa na serikali kuendeleza ruzuku ya petroli

January 24th, 2024 1 min read

NA JOHN MUTUA

SHIRIKA la Fedha Duniani (IMF) limeisuta Kenya kuhusu kuanzishwa upya kwa mpango wa ruzuku ya mafuta kwa misingi kwamba ukosefu wa fedha za kuwalipa wauzaji mafuta utavuruga bajeti.

IMF lilisema kuwa serikali ilianzisha tena ruzuku hiyo licha ya ukosefu wa fedha za kulipa wauzaji mafuta na Hazina kukosa kulipa kampuni hizo angalau Sh9 bilioni ambazo zimekusanya kutoka mwaka jana.

Rais William Ruto aliapa mwaka wa 2022 kwamba utawala wake hautatoa ruzuku kwa bei ya mafuta, kulingana na masharti ya kupata mikopo ya mabilioni ya pesa kutoka kwa taasisi ya Bretton Woods.

Mnamo Octoba 15, mwaka jana, lita moja ya petroli na dizeli ilikuw aikiuzwa kwa Sh217.36 na Sh205.47 mtawalia jijini Nairobi huku ruzuku hiyo ikizuia bei kupanda hadi Sh220.43 na Sh217.11 mtawalia.

Lakini IMF halikupokea vyema ujumbe wa kutolewa kwa ruzuku, ikizingatiwa kwamba kuondolewa kwake ilikuwa moja ya masharti mapya yaliyowekwa na mfadhili kama sehemu ya mpango wa msaada wa bajeti wa miezi 38.

“Mchakato mrefu wa kuunda jopokazi na uchapishaji wa uamuzi wake (mapitio ya bei ya mafuta ili kuhakikisha maamuzi yanawiana na fedha zilizopo) ilisababisha kuchelewa kwa utekelezaji wa Benchmark ya Kimuundo,” IMF ilisema.

“Hii inaakisi hitaji la mashauriano ya ndani kuhusu jinsi ya kufadhili maamuzi ya hivi majuzi ya bei ya ndani mnamo Oktoba 15 na Novemba 15.”

Kuondolewa kwa ruzuku hiyo mnamo Mei mwaka jana kulifanya bei ya mafuta kufikia viwango vya juu vya Sh182.70 na Sh168.40 kwa lita ya petroli na diseli mtawalia.

Kisha bei ikapanda hadi Sh200 baadaye mwakani kutokana na mseto wa kuondolewa kwa ruzuku na kuongezeka kwa Ushuru wa VAT kwa bidhaa za petroli hadi asilimia 16, na kulazimisha utawala wa Dkt Ruto kurejesha ruzuku hiyo.