Habari za Kitaifa

Inspekta jeuri anayekaidi sheria anazotaka raia wazitii

September 17th, 2024 3 min read

MAWIMBI na dhoruba kali za jela zimeendelea kuvuma kumwelekea Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli hasa baada ya kudharau na kuhujumu idara ya mahakama.

Jaji Mkuu Martha Koome amekemea kitendo cha kumpokonya dereva na mlinzi Jaji Lawrence Mugambi aliyemsukuma gerezani miezi sita kinara huyo wa polisi kwa kudharau na kukaidi maagizo ya korti.

Jaji Koome alisema kutwaa silaha za dereva na mlinzi wa Jaji Mugambi ni “kumhangaisha na kulipiza kisasi kwa kumfunga jela Masengeli”

Jaji Koome alisema Jumatatu kwamba tume ya kuajiri watumishi wa idara ya mahakama JSC haitakaa kitako huku majaji na mahakama wakiendelea kuuziwa woga na asasi nyingine za serikali.

Mnamo Ijumaa Masengeli alihukumiwa kifungo cha miezi sita kwa kudharau mahakama  na kukaidi maagizo awafikishe kortini wanaume watatu waliotekwa nyara wakati wa maandamano ya GenZ  Kitengela, Kaunti ya Kajiado.

Mbali na kutimuliwa wasimlinde Jaji Mugambi, maafisa hao wawili wa polisi walipokonywa silaha zao siku chache baada ya Bw Masengeli kuhukumiwa.

Jaji Mugambi alimfunga Bw Masengeli Septemba 13,2024 kwa kukaidi maagizo ya mahakama mara saba.

Alikuwa ameagizwa Agosti 26, 2024 afike kortini kueleza waliko mwanaharakati Bob Micheni Njagi na ndugu wawili Jamil na Aslam Longton .

Watatu hao walitekwa nyara Agosti 19, 2024 Kitengela, kaunti ya Kajiado baada ya maandamano ya Gen Z. Kufikia leo hawajulikani waliko.

Kitend

Jaji Mkuu Martha Koome. PICHA | RICHARD MUNGUTI

o hiki cha kumpokonya Jaji Mugambi mlinzi na dereva wake, kilifichuliwa Jumatatu (Septemba16) alasiri na Jaji Mkuu Martha Koome katika Mahakama ya Juu alipohutubia wanahabari.

Jaji Koome alilaani vikali kitendo hiki cha mafisa wakuu wa polisi akisema,“ni tisho kwa idara ya mahakama na hakiwezi kustahimiliwa.”
Jaji Koome alisema mlinzi na dereva wa Jaji Koome ambao ni maafisa wa polisi waliagizwa wafike mara moja katika makao makuu ya polisi kupewa mwelekeo na maagizo upya.

 

Jaji Koome alisema wawili hao walipofika kwa wakuu wao walipokonywa silaha za kupewa majukumu mengine.

Jitihada za JSC kuwarejesha hazikufua dafu kwa vile hakuna mtu hata mmoja aliyejibu ombi hilo.

“Hatua hii ni ushambulizi, uvurugaji wa uhuru idara ya mahakama na ukiukaji wa hali ya juu wa sheria.Walinzi wa majaji ni sehemu ya marupurupu na kamwe hawawezi kuondolewa au kutwaliwa,” Jaji Koome alisema katika Mahakama ya Juu Nairobi Jumatatu.

Akitaja kisa hiki kama hatua ya kuwatisha majaji, Jaji Koome aliitaka

Koome National Police Service irejeshe mara moja mlinzi na dereva wa Jaji Mugambi.

“Hatua ya kumpokonya jaji dereva na mlinzi baada ya uamuzi ambao hakuwafurahisha wakuu Fulani ni jambo la kusikitisha mno na kufadhaisha. Ni ujumbe wa kuhofisha sio tu kwa majaji mbali kwa wananchi wote kwa vile maafisa waliotunukiwa jukumu la kuhakikisha haki imo kwa kila mmoja wanaweza kutishwa na kudhulumiwa kwa sababu ya maamuzi yao au msimamo wao,” alisema Jaji Mkuu.

Jaji Koome aliongeza kwamba kisa hiki kitawafanya wananchi na umma kwa jumla kukosa imani na idara ya mahakama, kuhujumu demokrasia na asasi za serikali , utovu wa nidhamu na maasi ya sheria.

Jaji Mugambi alimfungu Bw Masengeli miezi sita kwa kukaidi maagizo ya mahakama kuhusu watatu hao.

Alitakiwa kufika kortini kueleza waliko na hatua zilizochukuliwa kuwatafuta.

Kwa mujibu wa familia za watatu hao,watu wanaoaminika kuwa maafisa wa polisi waliwateka nyara na kuwaingiza ndani magari yenye rangi nyeupe na kuchomoka nao kwa mwendo wa kasi.

Wiki iliyopita Jaji Mugambi alimwagiza Bw Masengeli ajisalimishe kwa Kamishna wa Idara ya Magereza (KPS) kuanza kutumikia kifungo cha miezi sita.

“Endapo Bw Masengeli hatajisalimisha kwa Kamishna mkuu wa KPS, Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki ahakikishe Bw Masengeli ametumikia kifungo,” Jaji Mugambi aliagiza.

Hata hivyo Jaji Mugambi alimpa fursa ya kuhepa kutoswa jela kwa kufika kortini kueleza waliko wanaume hao watatu.

Akifika kortini na kuomba msamaha huenda kifungo hicho kikafutiliwa mbali ama kutozwa faini.

“Kitendo cha kuwapokonya mlinzi na dereva wa Jaji Mugambi silaha ni hatua ya moja kwa moja kuhujumu mahakama. Huku ni kudhihaki sheria na katiba,”Jaji Koome alisema.

Jaji huyo mkuu alisema Kifungu nambari  160 cha Katiba kinalinda uhuru wa Mahakama, na kwamba Idara hii haidhibitiwi ama kupewa maagizo na mtu yeyote yule.

“Walinzi wa majaji ni haki yao na haipasi kuondolewa kiholela jinsi ilivyofanywa,” Jaji Koome alisema.

Kamanda wa Idara ya Ulinzi wa Maafisa wakuu serikalini na ulinzi wa majengo ya serikali (SGB/VIP) Bw Lazarus Opicho alikuwa ameagizwa afike kortini Septemba 13, 2024 kueleza sababu ya kuwapigia simu dereva na mlinzi wa Jaji huyo kuwahoji alikokuwa Septemba 9,2024.

Alifika kortini na kuomba msamaha.

Mawakili Cecil Miller na Danstan Omari wanaomwakilisha Masengeli wamekata rufaa.

Kesi ya Masengeli ya itatajwa mbele ya Jaji Enock Mwita Septemba 19,2024 kwa maagizo zaidi.