Habari za Kaunti

Jinsi vijana, kina mama 10,000 watanufaika kiuchumi Mombasa

Na WINNIE ONYANDO September 19th, 2024 2 min read

TAASISI ya Mama Haki imeanzisha awamu ya pili ya mpango unaolenga kuwainua akina mama na vijana 10,000 kimapato.

Mpango huo wa miaka mitano unalenga kuwapa vijana na akina mama katika Kaunti ya Mombasa ujuzi wa kifedha, utaalamu wa kidijitali, ujasiriamali, na ujuzi unaohitajika kwa maendeleo ya kiuchumi.

Mamia ya wakazi wa Mombasa Septemba 18, 2024 walihudhuria kongamano hilo lililofanyika katika Kituo cha Rasilimali cha Licodep kilichopo katika Kaunti Ndogo ya Likoni, Mombasa.

Seneta mteule Miraj Abdillahi, aliwapongeza washirika wa mpango huo kwa hatua yao kuendeleza lengo hilo adhimu, akiongeza kuwa utawapa walengwa ujuzi wa kisasa kama vile utumizi wa akili mnemba – Artificial Intelligence (AI), kompyuta, uundaji wa programu za simu, na elimu kuhusu matumizi ya kifedha.

“Kongamano hili linatufunza kuwa hakuna lisilowezekana miongoni mwa vijana na akina mama Mombasa. Kando na kumwezesha mtu binafsi, tunaanzisha harakati ya ukuaji wa kiuchumi unaoongozwa na wanawake,” alisema seneta huyo mteule.

Meneja wa Mauzo wa Benki ya DTB Kenya Kanda ya Pwani, Mercy Douglas, alisema benki hiyo imejikita katika kubadilisha maisha ya watu na kuona wachuuzi pamoja na wafanyabiashara wadogo wakipata ujuzi na rasilimali za kupanua biashara zao kwa kiwango kipya.

“Hatufundishi tu ujuzi wa biashara; tunajenga biashara zitakazoongozwa na wanawake ambazo zitabadilisha uchumi wa Mombasa. Tunataka kuona hawa wanawake na vijana wakitoka kwenye biashara za kijadi na kuwa wakurugenzi wakuu wa kampuni kubwa ndani ya miaka mitano ijayo,” alisema Mercy.

Taasisi ya Mama Haki pia imezindua mpango wa kipekee wa ushauri, unaowaunganisha walengwa na wanawake wajasiriamali waliobobea kutoka kote nchini, ili kuimarisha uchumi.

Mpango huo utahusisha warsha za kina zitakazoongozwa na wataalamu wa viwanda, ambapo washiriki watahusika katika miradi ya vitendo inayolenga kutatua changamoto za kijamii katika ngazi ya ndani.

Mpango huu unaendana na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), Dira ya Maendeleo ya 2030, na Ajenda ya Rais William Ruto ya ustawishaji uchumi Botton Up Economic Transformation Agenda ambayo inalenga kuboresha maisha ya Wakenya.