Habari za Kitaifa

Joho amenyamana na asasi za serikali zinazolemaza miradi ya ufugaji samaki

Na VICTOR RABALLA August 22nd, 2024 1 min read

WAZIRI wa Madini, Uchumi wa Majini na Masuala ya Bahari, Bw Ali Hassan Joho, amelaumu mashirika mengine ya serikali kwa kutatiza ujenzi wa Kituo cha Huduma na Mafunzo ya Kilimo cha Uvuvi cha Kabonyo kwa gharama ya Sh2.5 bilioni eneo la Nyando, Kaunti ya Kisumu.

Licha ya fedha kupatikana kwa mradi huo wa mabilioni, Waziri huyo alishtumu maafisa wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kusimamia Mazingira (Nema) na Mamlaka ya Kitaifa ya Ujenzi (NCA) kwa kuhujumu mradi huo uliozinduliwa na Rais William Ruto Oktoba 6, 2023.

“Tayari tumepata mwanakandarasi na kutia saini, tumekamilisha miundo na fedha zilitolewa na serikali ya Hungary. Kwa bahati mbaya, hatukuweza kuanzisha mradi huu kutokana na vizingiti vilivyowekwa na maafisa wa Nema na NCA,” alisema Jumanne, Agosti 20, 2024 wakati wa ziara rasmi mjini Kisumu.

Katika juhudi za kupata idhini kutoka kwa Nema na NCA, Bw Joho alisema mwanakandarasi huyo mpya alizungushwa kutoka afisi moja hadi nyingine na kuchelewesha ujenzi wa mradi huo unaolenga kuimarisha uvuvi katika eneo hilo.

Waziri huyo aliagiza afisi hizo mbili kuwezesha mwanakandarasi huyo kuanza mradi huo wiki hii kabla ya ziara ya Rais Ruto katika eneo la Nyanza wiki mbili zijazo.