Makala

Kampeni ya Gachagua watu kuzaana yapata pingamizi

June 7th, 2024 3 min read

NA MWANGI MUIRURI

KAMPENI za Naibu Rais Rigathi Gachagua za kuwahimiza wenyeji wa Mlima Kenya wazaane kwa wingi zimepata pingamizi kutoka kwa wataalamu wa upangaji uzazi, kiuchumi na pia baadhi ya wenyeji.

Katika kampeni hiyo ya Bw Gachagua ambayo tayari imekumbatiwa na wabunge kama Edwin Mugo wa Mathioya, Bi Mary wa Maua wa Maragua na Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu, ambao huonekana kwa mikutano wakitoa pesa kwa walio na uja uzito huendeshwa kwa msingi kwamba “wingi wetu ndio uthabiti wetu na tukipungua tutamezwa na wengine”.

Bw Gachagua husisitizia wenyeji kwamba idadi yao ndiyo thamani yao katika siasa na bima yao dhidi ya kudharauliwa kwa kuwa wote walio mamlakani huheshimu na kutii mito ya walio wengi.

“Kabla ya tuambiwe sisi tuzaane, napendekeza kwa unyenyekevu kwamba kwanza tufanyiwe harakati za kuhesabiwa kisha tusajiliwe upya kulingana na viwango vya utajiri wetu. Wale ambao ni mabilionea na mamilionea kama Bw Gachagua kwanza wawekewe amri ya kuzaa watoto zaidi ya 100 na wawe huru kuoa wake wengi iwezekanavyo kuafikia uzazi huo. Ikiwa uzee umewaandama na hawawezi wakawapata, waagizwe wachukue mayatima na watoto wa mitaani walee,” akasema mshirikishi wa masuala ya vijana ukanda wa Mlima Kenya Bw Gitau Warui.

Bw Warui alisema kwamba wengi wa mabwanyenye katika biashara na siasa eneo la Mlima Kenya huwa na watoto wasiozidi watatu “lakini Bw Gachagua anatwambia sisi wa huku chini tuzae watoto zaidi ya 10”.

Mtaalamu wa masuala ya kiafya ambaye ndiye afisa msimamizi wa kitengo cha afya-mitandaoni (e-health) Bw Onesmus Mwaura anasema kwamba suala la uzazi na maendeleo ya nchi huenda sambamba.

“Ndio sababu huwa tunahesabu watu walio hapa nchini kila baada ya miaka 10 huku tukihimiza idadi ya wakimbizi wanaoingia nchini wathibitiwe ndio tuandae mipango ya rasilimali zetu kulingana na uwezo wetu. Familia zinafaa kuzaa watoto ambao wanaambatana na uwezo wa mlezi au walezi kwa kuwa ukizaa wenye huwawezi, utatwika wakenya wengine mzigo wa kuwalea ukijua vizuri hawakuwa washirika wa tendo lako la ngono lililoishia mimba hizo,” asema.

Anaongeza kwamba “zaa wale ambao utaweza kulisha, kupea afya bora, kuwapa makao, kuelimisha na pia kuwaachia urithi kwa kuwa kusema mtoto huja na mali yake ni usemi wa kukubali umaiskini kimakusudi”.

Alisema “umasikini hukadiriwa kupitia ukosefu wa uwezo wa kuishi maisha bora na aibu kubwa ni uwe maisha yako ni duni na kisha unaongeza dunia watoto ambao hujui malezi yao yatafathiliwa kutoka mfuko wa nani, sio tu familia yako unaumiza bali pia ukoo, jamii na taifa kwa ujumla”.

Alisema hali hiyo ndiyo hufanya taifa liingie hata kwa mikopo kiholela “tukijaribu kusaka rasilimali za kugharamia bajeti ambazo zingeafikiwa katika familia huku msukumano wa masikini wakisaka lishe ukitutwika jinamizi ya utovu wa kiusalama na kuporomoka kwa maadili”.

Katibu Mkuu wa Shirika la Wanawake Waelimishaji barani Afrika (Fawe-K) Bi Cecilia Wanjiku alisema watoto wengi ni wa maana wakati tu hawatatizi uthabiti na ubora wa familia, kesho ya watoto hao imehakikishiwa kwamba haitakuwa ya taabu zinazoweza kuepukika na pia hawazoroteshi afya ya mama anayewazaa.

Bi Wanjiku alisema kwamba kwa sasa “shida tuliyo nayo ni ya wanasiasa kufikiria kwa msingi wa kura za chaguzi zijazo pasipo kufikiria suala la kiuchumi katika familia na nchi”.

Alisema “moyo wangu unasononeka kuwapata wanasiasa katika majukwaa ya hadharani wakiwaambia waja wazito wapige foleni wakabidhiwe Sh500 kama zawadi”.

Alisema ni vyema kuwatuza wanawake pesa “lakini isiwe ni kwa hadaa kwamba pesa hizo zinatosha kulea mwana huyo hadi kesho yake”.

Aliwataka wenyeji wa Mlima Kenya wapevuke macho na wawe na upana wa kimawazo wa kudadisi masuala kwa njia inayowapa kinga dhidi ya mito ya umasikini.

“Ukimzaa mtoto huyo jiulize kama utampa mahitaji ya kimsingi na amenyanie nafasi za uongozi wa nchi sawa na wale wa mabwanyenye ambao hutuma watoto wao hadi shule za ulaya kujipa makali ya kuongoza nchi na kuendesha biashara, huku wako wewe masikini ukiambiwa wapande maparachichi na wafuge sungura ndio wapate lishe,” akasema.