Habari Mseto

Kampuni za mTek na BuuPass zaungana kutoa bima kwa abiria

Na LEONARD ONYANGO August 5th, 2024 1 min read

ABIRIA sasa wanaweza kupata bima ya kuwakinga iwapo watapata ajali na kujeruhiwa au mizigo yao kuharibika.

Hii ni baada ya mTek, kampuni inayowezesha Wakenya kulinganisha, kuchagua na kununua bima kidijitali, kuungana na kampuni ya BuuPass inayowezesha abiria kununua tiketi ya basi kwa njia ya mtandao.

Kupitia bima hiyo, abiria analipwa fidia mizigo yake inapoharibika au kulipiwa gharama ya matibabu anapojeruhiwa ajali inapotokea.

Kulingana na Mkurugenzi wa mTek Bente Krogmann, bima hiyo ni afueni kwa abiria ambao wamelazimika kuhangaika kutafuta hela za matibabu wanapopata ajali.

“Abiria anaponunua tiketi ya basi katika mtandao wa BuuPass anaweza kuchagua kulipia bima ya kumkinga anaposafiri. Bima hiyo ni muhimu kwani itakuwa ya manufaa makubwa ajali inapotokea,” akasema Sonia Kabra, Mkurugenzi wa BuuPass.

Idadi kubwa ya Wakenya wanaosafiri umbali mrefu hutumia mabasi ambayo tiketi zake zinapatikana katika mtandao wa BuuPass.

Kulingana na Ripoti ya Hali ya Uchumi Nchini ya 2024 iliyotolewa na Shirika la Takwimu Nchini (KNBS), watu 12,000, wakiwemo madereva 2,075, walihusika katika ajali za barabara zilizohusisha mabasi au matatu ambapo jumla ya watu 1,100 waliangamia.