Habari za Kitaifa

Kanisa la Mackenzie ni kundi la uhalifu – Serikali

January 31st, 2024 1 min read

NA ALEX KALAMA

WAZIRI wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki amechapisha kwenye gazeti rasmi la serikali kwamba Kanisa la mhubiri tata Paul Mackenzie la Good News International ni kundi la uhalifu.

Prof Kindiki amechukua hatua hiyo mnamo Jumatano, kufuatia kupokea dokezo na ripoti mbalimbali kuhusu mauaji yaliyotokea katika msitu wa Shakahola ulioko Kaunti ya Kilifi.

Inadaiwa kwamba Bw Mackenzie na watu wengine alioshirikiana nao, walitoa mafundisho ya kupotosha ambapo waumini kadhaa wa Kanisa hilo walishawishika kufunga hadi kufa kwa kisingizio kwamba wangepata fursa ya kukutana na Yesu.

“Kwa mujibu wa mamlaka niliyopewa katika Sehemu ya 22/1 ya Sheria ya Kuzuia Uhalifu Uliopangwa, ninatangaza kwamba dhehebu la Good News International Ministeries ni kundi la wahuni waliojipanga kwa ajili ya kutekeleza vitendo vya kinyama,” amesema waziri Kindiki.

Inadaiwa mafundisho tata ya kundi hilo yalichangia vifo vya watu zaidi ya 400.

Kwa sasa kiongozi wa dhehebu hilo tata la Good News International bado anazuiliwa katika gezera la Shimo la Tewa yeye pamoja na wenzake.

Mwanzoni mwa Januari 2024 Mahakama Kuu ya mji wa Malindi ilitoa agizo kwamba Bw Mackenzie pamoja na washirika wake zaidi ya 30 walioshtakiwa kwa kesi ya mauaji kufanyiwa uchunguzi wa akili kabla ya kuanza kusikilizwa kwa mashtaka dhidi yao.

Bw Mackenzie pamoja na wenzake zaidi ya 30 wanakabiliwa na mashtaka 191 ya vifo vya watoto 191 vilivyotokea msituni Shakahola.

Kesi hiyo inatarajiwa kuanza rasmi Februari 6, 2024, katika mahakama hiyo ya Malindi.