Habari Mseto

Kanisa la PCEA lampoteza mzee Johana Nyutu

May 25th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

KANISA la Kipresibeteria (PCEA) katika Kaunti ya Kiambu linaomboleza kumpoteza mzee Johana Nyutu Kariuki ambaye katika uhai wake alisifika sana kwa kueneza imani ya dhehebu hilo mashinani.

Mbunge wa Githunguri Bi Gathoni Wamuchombna akihutubu katika mazishi ya mwendazake katika kiijiji cha Wanjenga, alisema serikali ingekuwa na wito wa kujituma katika huduma sawa na za mwendazake wakati wa uhai wake, basi taifa hili lingekuwa limepiga hatua hata za kukopesha pesa mataifa yaliyostawi.

“Huyu ni mzee ambaye waliomjua wanatambua alikuwa mtu wa kujitolea katika kueneza na kuhimiza maadili mema katika jamii na kuwataka watu kumtii Mungu. Pia alikuwa akihimiza jamii kuwa na bidii ya mchwa kujistawisha kirasilimali,” akasema Bi Wamuchomba.

Marehemu Kariuki ni mzazi wa Bi Jane Wanjiru ambaye ni mke wa mwandishi wa habari wa miaka mingi Bw Joseph Kamutu, ambaye huhudumu katika kitengo cha mawasiliano cha serikali.

Bi Wanjiru Kamutu, ambaye ni mke wa mwandishi wa habari wa muda mrefu Bw John Kamutu, aongoza wengine kumpa heshima za mwisho babake mzazi – Mzee Johana Nyutu Kariuki. PICHA | MWANGI MUIRURI

Bi Wanjiru aidha ashawahi kuhudumia taifa ambapo alikuwa diwani maalum katika manispaa ya Nyeri, kabla ya serikali za kaunti kutua mwaka wa 2013.

“Ni masikitiko makuu kwamba tumempoteza mzee wetu ambaye alikuwa hamasisho letu kuu kuhusu maadili na bidii. Mungu amemuita nyumbani akapumzike akiwa na umri wa miaka 83 na ambapo msukumo wa damu na ugonjwa wa kisukari ndizo zimepambana kumpumzisha,” akasema Bw Kamutu.

Bw Kamutu alisema kwamba mzee Kariuki ndiye alianzisha kanisa la PCEA la Githima ili kuwapa wenyeji dhehebu la kumtukuza na kumlilia Mungu katika imani yao.

Pasta msimamizi wa Gathugu, Bi Leah Kamunya, akiongoza misa ya mazishi alisema kwamba kanisa hilo limempoteza shujaa wa imani na muumini sugu wa itikadi za Kikirsto.

“Kupitia kuwakuza kiimani watu wa familia yake, aliweza kuwashawishi Prof Peter Kariuki na Bi Esther Wainaina kuwa wainjilisti wasifika katika kanisa hili. Bi Wainaina kwa sasa akiwa ndiye msimamizi wa masuala ya imani katika Chuo Kikuu cha Kenyatta. Aidha, watoto wake wawili ambao ni Bi Jane Kamutu na pia Ronah Karanja ni Wazee wa Kanisa, hali ambayo hata nikiwa hapa kuongoza misa hii ya mwendazake najivunia kwamba tunamzika mtu ambaye alikuwa ni kielelezo bora kwetu,” akasema Bi Kamunya.

Mazishi ya Mzee Johana Nyutu Kariuki. PICHA | MWANGI MUIRURI