Habari Mseto

Kaunti ya Nairobi kuwaajiri askari 800

November 14th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Baraza la jiji linalenga kuwaajiri askari 800 zaidi kwa lengo la kutekeleza sheria na kanuni za Jiji la Nairobi.

Serikali ya Kaunti ya Nairobi ilisema katika ripoti kuwa ukosefu wa askari wa kutosha umeathiri utekelezaji wa sheria, ikiwemo ni pamoja na marufuku ya bodaboda katikati mwa jiji.

Serikali hiyo itatumia Sh600 milioni kufikia 2020 kuajiri na kuwapa mafunzo wahudumu wapya ambao inatarajia kutumia kuimarisha juhudi za kutekeleza sheria jijini.

Idadi ya askari wa baraza la jiji sio wazi, lakini Januari, aliyekuwa akisimamia idara hiyo Peter Mbaya alisema kulikuwa na skari 97.

“Serikali ya kaunti itaajiri askari 800 katika mwaka wa kifedha wa 2018-19 kwa lengo la kuongeza idadi ya wahudumu,” ilisema City Hall katika mpango wake wa kifedha.

Kulingana na baraza hilo, wahudumu walioko wameshindwa kukabiliana na watu wanaorusha taka ovyo ovyo, wachuuzi na biashara zinazohudumu bila leseni.