Michezo

KBC yakemewa kwa upeperushaji mbovu wa Afcon

January 17th, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI

MASHABIKI wanaofuatilia na kutazama mechi za kipute cha Timu Bora Afrika (Afcon) kinachoendelea nchini Ivory Coast wamelalamika kuhusu upeperushaji mbovu katika runinga wakitaka Shirika la Utangazaji Nchini (KBC) kuboresha mitambo yake.

KBC ambayo inamilikiwa na serikali ndiyo tu iliyo na hatimiliki za kupeperusha dimba hilo lakini katika siku tatu za kwanza, mitambo imekuwa ikianguka ovyoovyo.

“Ni nini hii sasa? Ama picha zimekwama au sauti ina mkwaruzo. Mara nyingine hakuna picha kabisa na mara nyingine hata televisheni inapoa ni kama hakuna chochote,” akalalama shabiki mmoja aliyepiga simu katika idhaa ya Kiswahili ya KBC, Radio Taifa mnamo Jumatatu jioni wakati wa mchuano kati ya Senegal na Gambia.

Hali ilikuwa mbaya hadi KBC ikaleta marudio ya mechi za awali wahandisi wake wakisaka mbinu ya kutuliza hali.

Shabiki huyo aliteta kwamba “ni kama hamtaki tushuhudie Taifa la Tanzania linalowakilisha Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) likiinua kombe hilo na kisha kujishidia zawadi ya Sh1 bilioni iwapo litaibuka bingwa”.

Satelaiti za Shirika la Utanzaji Nchini (KBC) zilizo katika eneo la Mai Mahiu katika barabara ya Narok-Mai Mahiu katika hii picha ya Aprili 30, 2015. PICHA | MAKTABA

Waliomjibu shabiki huyo walisema shida iko katika miundombinu ya taifa la Cote d’Ivoire lakini sio hapa nchini wala katika mitambo yao “kwa kuwa ukiangalia vipindi vyetu vingine viko sawa”.

Shida hiyo ya kimitambo aidha iliathiri matangazo katika redio kwa kuwa watangazaji pia walikumbana na hitilafu hiyo.

Watangazaji hao wakiwa hapa nchini, hutazama runinga kisha wanatangaza mitanange hiyo.

Waziri wa Michezo Ababu Namwamba alikuwa ameahidi Wakenya kwamba runinga ya KBC ilikuwa na uwezo wa kupeperusha mechi zote 54 zikishirikisha mataifa 24 kati ya Januari 13 hadi Februari 11, 2024.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa KBC Bw Paul Gitau alikuwa amesema “tutajiangazia kama wababe wa upeperushaji kipute hicho hadi mashabiki waridhike”.

Mashabiki wengi sasa wanataka waratibu wa matangazo hayo ya mpira watafute mbinu ya kuhakikisha upeperushaji usio na hitilafu hizo.

[email protected]