Habari

KDF wateka mtaa Mombasa

August 16th, 2019 2 min read

Na HAMISI NGOWA

WANAJESHI wa kikosi cha Majini cha KDF (Kenya Navy) Jumanne usiku waliteka mtaa wa Mtongwe katika eneo la Likoni, Kaunti ya Mombasa na kuwatandika wananchi pamoja na polisi.

Wanajeshi hao waliwavamia na kuwajeruhi wakazi wengi kulipiza kisasi mauaji ya mmoja wao, Koplo David Mwangi Githinji, ambaye mwili wake ulipatikana mtaani humo Jumamosi iliyopita.

Maafisa watatu wa polisi na mmoja wa Shirika la Kulinda Wanyapori (KWS) walijeruhiwa pia kwenye uvamizi huo uliodumu kutoka saa mbili jioni hadi usiku wa manane.

Wanajeshi hao kutoka makao Makuu ya Jeshi la Majini (Navy) ya Mtongwe, waliingia mtaani humo kwa malori ya kijeshi wakiwa wamejihami kwa silaha kali, wamevalia sare rasmi na kufunika nyuso kama waliokuwa wanaenda kupambana na jeshi kubwa la maadui.

Walipofika walijigawa katika makundi na kuanza kumtwanga kila waliyekutana naye, wakitaka waelezwe ni nani aliyeua mwanajeshi mwenzao.

Wakazi wanasema wanajeshi hao waliokuwa na bunduki, marungu, panga na silaha butu, walihangaisha wakazi katika maeneo ya Wimbini, Midodoni, Grand, Mweza na Vijiweni ambako raia walilazimika kujifungia kwenye nyumba zao ili kuepuka kichapo huku vilio na mayowe zikitawala.

Hamisi Salim Koka, ambaye ni dereva wa bodaboda katika eneo hilo, alisimulia Taifa Leo alivyopokea kichapo cha mbwa kutoka kwa maafisa akiwa kwenye shughuli zake za kusafirisha abiria.

Bw Koka, ambaye aliumizwa vibaya mkono wake wa kulia, anasema alikamatwa saa mbili usiku na maafisa sita wa jeshi. Maafisa hao walimpiga na kumtaka awaseme washukiwa waliohusika na mauaji ya mwenzao.

“Niliumia mkono pamoja na ubavu na nina maumivu makali,” akasema Bw Koka.

Hatua chache kutoka nyumba ya Bw Koka, waathiriwa wengine wawili – Mbwana Saidi na mwenzake walisema zaidi ya wanajeshi 10 waliingia kwenye nyumba yao mwendo wa saa mbili za usiku na kuwapiga vibaya.

Saidi alipata majeraha kwenye mguu na akakimbizwa hospitali ya wilaya ya Likoni ambako alitibiwa.

Afisa wa KWS aliyeumizwa alisema wanajeshi hao walimtandika hata baada yake kujitambulisha.

“Nilikuwa nimetoka kazini dereva wa bodaboda aliyekuwa amenibeba aliposimamishwa na kuanza kucharazwa vibaya bila sababu. Hata baada ya kujitambulisha kuwa mimi ni afisa wa KWS waliendelea kunitwanga,” akasema afisa huyo.

Viongozi wa eneo hilo walikashifu kitendo hicho, na kutaka serikali iwachukulie hatua waliohusika.

Mbunge wa zamani wa Likoni, Bw Suleiman Shakombo, alitaka kujua kwa nini wanajeshi hao walitoka kwenye kambi yao bila amri ya Amiri Jeshi Mkuu.

“Sijui wanajeshi walipata wapi mamlaka hayo ya kuwapiga raia. Hicho ni kinyume cha sheria na twaomba waliohusika katika kupiga watu wa kuwajeruhi waweze kuchukuliwa hatua za kisheria,’’ akasema.

Diwani wa eneo hilo, ambaye ni Kiongozi wa Wengi katika bunge la Kaunti ya Mombasa, Bw Hamisi Musa Mwidani, alisema wanajeshi walikosea kwa kuchukua kazi ya polisi.

“Ikiwa kuna mwanajeshi aliyeuawa, ilikuwa kazi ya polisi kufanya uchunguzi na kumkamata aliyehusika. Ni makosa kwa wanajeshi kutoka kwenye kambi yao na kuanza kupiga watu,’’ akasema.