Habari Mseto

KeNHA yafunga barabara ya Garissa-Madogo kutokana na mafuriko

April 27th, 2024 1 min read

NA CHARLES WASONGA

MAMLAKA ya Kusimamia Barabara Kuu Nchini (KeNHA) imefunga sehemu ya barabara kati ya Garissa na Madogo, katika eneo la Kaskazini Mashariki mwa Kenya kufuatia mafuriko makubwa.

KeNHA lisema hatua hiyo imechukuliwa kufuatia mafuriko yaliyoshuhudiwa karibu na daraja la Tana River, maeneo ya Mororo na Kona Punda.

“KenNHA ingependa kujulisha umma kuwa barabara kati ya Garissa na Madogo imefungwa kwa watumiaji wote wa barabara hadi viwango vya maji vishuke na kazi ya kukarabati sehemu iliyoharibika kuisha. KeNHA itaendelea kufuatilia hali,” taarifa ya KeNHA ikasema.

Kulingana na mamlaka hiyo, itaendelea kufuatilia hali na itatoa mwelekeo baadaye.

KeNHA iliwahakikishia watumiaji barabara hiyo kwamba wataruhusiwa kuitumia baada ya sehemu iliyoharibika kukarabatiwa.

Mamlaka hiyo imekuwa ikitoa habari kuhusu hali ya mafuriko nchini huku ikionya watumiaji barabara kuwa waangalifu katika maeneo yaliyoathirika na mafuriko pamoja na maporomoko ya ardhi.